Lindi. Naibu Waziri wa Afya, Faustine Ndugulile ameutaka uongozi wa wilaya Nachingwea mkoani Lindi kukaa pamoja ili kutatua changamoto za kiutendaji zinazosababisha kukwamisha ukarabati wa hospitali ya wilaya hiyo na vituo vya afya.
Dk Ndugulile ameyasema hayo leo Septemba 8 alipotembelea Hospitali ya Wilaya na kubaini utendaji usioridhisha ikiwemo utunzaji duni wa dawa, uchafu wa mazingira na ucheleweshaji wa ukarabati wa hospitali hiyo.
“Utendaji na usimamizi mbovu wa mambo ni miongoni mwa kasoro zilizopo hapa,” amesema.
Amesema amebaini pia udhaifu katika utunzaji wa kumbukumbu za dawa na rekodi za kuingia na kutoka kwa vifaa tiba.
Amesema ingawa serikali imepeleka Sh400 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali hiyo lakini hakuna kilichofanyika.
“Hali hii inakwamisha nia njema ya serikali ya kuwahudumia wananchi wake ambao ndio walipa kodi na wadau wakubwa wa maendeleo na uchumi wa nchi,” amesema.
Pia Ndugulile ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha eneo la hospitali hiyo linakuwa safi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Samuel Laizer amesema kuchelewesha kwa ukarabati wa hospitali kumetokana na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kuwa na urasimu.
“Nimejaribu kumshauri zaidi ya mara mbili kwa maandishi lakini amekuwa akiendelea na msimamo wake na kudai kwamba anatafuta mkandarasi mwenye uwezo ,” amesema