Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu awataka wanaume kupima Ukimwi

11413 Ukimwi+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wanaume wote wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakapime afya zao ili kubaini kama wameambukizwa virusi vya Ukimwi au la.

Ametoa rai hiyo jana Ijumaa Julai 13, 2018 wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

“Napenda kusisitiza kwa akinababa wote kwamba ukimwi bado upo na wanaume hamuendi kupima, ni wagumu kwenda kupima eti kwa sababu mnawategemea wake zenu waende kupima,” amesema.

“Unamwambia mama aende kupima akija na majibu ukajua hana maambukizi, wewe huku unashangilia kwamba uko salama. Hapana, nendeni mkapime kwa sababu kila mmoja na vyanzo vyake vya kupata maambukizi.”

Amesema maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika wilaya ya Kishapu yako kwenye asimilia 2.1 ikilinganishwa na kiwango cha maambukizi ya VVU kwa mkoa mzima ambayo kwa sasa ni asilimia tano.

“Ni vema familia zikapima VVU ili mjue hali zenu na muishi kwa furaha na kama kuna mmoja ameambukizwa basi aanze tiba mara moja,” amesema Majaliwa ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.

Pia, amewataka wakazi wa wilaya ya Kishapu wajiunge na bima ya afya ili waweze kupata tiba hata wakati hawana fedha.

“Halmashauri yenu imeweka kiwango cha Sh 30,000 kwa mwaka ambapo baba, mama na watoto wanne watakaojiunga na huduma hii ya afya ya jamii, watapata matibabu bure kwa muda wa mwaka mzima mahali popote.”

“Ninawaomba mjiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utakuwezesha kupata tiba siku ambayo huna hela mfukoni au nyumbani. Pia utakuwa na uhakika wa kupata matibabu bure kwenye zahanati au kituo cha afya chochote kile katika katika wilaya hii,” amesema.

Waziri Mkuu leo Julai 14, 2018 anaendelea na ziara yake wilayani Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz