Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu aonya wapotoshaji kuhusu chanjo

Majaliwa Pc Data Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa

Tue, 7 Sep 2021 Chanzo: Mwananchi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya watu wanaotoa maneno kuhusu chanjo ya maambukizi ya Uviko 19, akisema chanjo hiyo ni salama na ni tiba kwa wanaotumia.

Ameyasema hayo leo Septemba 7, 2021 wakati akihutubia katika mkutano wa wadau wa mifugo uliofanyika jijini Dar es Salaam, akieleza sababu ya Serikali huruhusu chanjo nchini.

“Chanjo hapa kwetu imekuwa na maneno maneno mengi. Nataka niwaambie tupunguze maneno, hii ni tiba na tiba hii mtu hawezi kuithamini mpaka limkute kwenye familia ndiyo atajua umuhimu wa chanjo,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema chanjo hiyo ni salama akisisitiza kuwa Serikali imeshajiridhisha.

“Viongoni wa Taifa hili kutoka mwaka 2020 ulipoingia ugonjwa huu kwa mara ya kwanza, walisema hatutaleta chanjo hapa na hatutachanja mpaka tujiridhishe.

Ameendelea kusema kuwa, baada ya Serikali kuona baadhi ya nchi duniani zinaweka masharti kwa wananchi wao ambao pia wanakuja kufanya biashara Tanzania waliona waruhusu chanjo.

“Chanjo hizi ni salama na tumejiridhisha. Tulipeleka wasomi wa Kitanzania kwenye udaktari, waliobobea kwenye sekta ya afya na wanathaminika na wanaatambulika ndani na nje ya nchi,” amesema.

Amesema kutokana na ugonjwa huo, baadhi ya mataifa yaliweka msharti yaliyowabana wananchi wao na hata Watanzania wanaoishi huko.

“Mheshimiwa Rais anajua pia hapa ndani kuna ndugu zetu ambao wamekuja kufanya shughuli zao lakini huko kwao wana masharti ya kuchanja wako hapa.

“Ilikuwa si busara tukawanyima fursa hiyo kwa kuzuia hiyo chanjo isiingie nchini. Mheshimiwa Rais akaridhia kwa ajili ya ndugu zetu wanaotoka Tanzania wachanje kwa ajili ya chanjo zao,” amesema.

Amesema pia kuna baadhi ya nchi zimeweka masharti ya watu wasiochanja kutoingia kwao, hivyo hakukuwa na sababu ya kuzuia.

“Kuna Watanzanjia wanafanya biashara huko, kuna Watanzania wanasoma huko au yeye anasoma huko ana ndugu anakwenda kusalimia na shughuli mbalimbali za kijamii. Lakini yuko tayari kuchanja, tukizuia tunashusha uchumi wake.

“Tukasema tuingize dozi anayetaka aende, ndiyo tukaingiza dozi milioni moja ambazo tunaendelea kuchanja. Lakini kuna Watanzania walikuwa wanakwenda Afrika Kusini kuchanja, wapo waliokuwa wanaona umuhimu, wengine walikuwa wanakwenda Nairobi, wengine Zanzibar."

Chanzo: Mwananchi