Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Jenista achangia ujenzi hospitali inayojengwa na wanakijiji

IMG 1 768x445 Waziri Jenista achangia ujenzi hospitali inayojengwa na wanakijiji

Sat, 9 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Jimbo la Peramiho ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameunga mkono jitihada za wananchi wa Kijiji cha Matimira B kilichopo jimboni kwake kwa kuchangia shilingi milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na shilingi milioni 1 ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji hicho.

Mhe. Jenista ametoa mchango huo katika Kijiji cha Matimira B, wakati wa ziara yake ya kuhimiza ushiriki wa wananchi katika maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii katika jimbo lake.

Mhe. Jenista amesema kuwa, akiwa ndiye Mbunge anayewawakilisha wananchi wa Jimbo la Peramiho katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameamua kuwa nao bega kwa bega katika masuala yote yanayohusu maendeleo.

Mhe. Jenista ametumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Neema Maghembe kuunga mkono kwa vitendo jitihada za wananchi pindi wanapoanzisha miradi ya maendeleo ya kijamii kama huo wa ujenzi wa zahanati.

“Wananchi hawa wamefyatua tofali wenyewe na kuziweka katika eneo la ujenzi, leo tunashiriki nao kuchimba msingi wa ujenzi wa zahanati, hivyo Mkurugenzi na watendaji wako hamna budi kuwaunga mkono ili kukamilisha zahanati hii kwa wakati na kuanza kutoa huduma,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista amesema kuwa, iwapo watajitokeza wadau wa maendeleo ambao wana nia ya kuunga mkono jitihada za wananchi wake yupo tayari kushirikiana nao ili kutimiza lengo la wananchi wa Matimira B la kukamilisha ujenzi wa zahanati itakayotoa huduma kwa akina mama, wazee, watoto, vijana na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Matimira B, Bi. Sylivia Mhagama amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Jenista Mhagama Mbunge kwa kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Zahanati hiyo ambayo itawapunguzia mzigo wa gharama ya kusafiri hadi Peramiho au Songea mjini kufuata huduma za afya.

Naye Bw. Filbert Nkale amesema Kijiji chao kimekuwa kikikabiliana na changamoto ya kukosa zahanati kwa kipindi kirefu, changamoto iliyosababisha akina mama kutopata huduma ya afya ya mama na mtoto hivyo kuhatarisha maisha yao.

Bi. Coltilda Komba, amemshukuru Mhe. Jenista kwa kuzindua ujenzi wa Zahanati ya Matimira B kwani itawawezesha kupata huduma ya afya ya mama na mtoto ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Mhagama ameanza ziara jimboni kwake yenye lengo la kuhimiza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live