Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Gwajima atoa siku 10 sakata mgonjwa aliyefumuliwa nyuzi

Gwajimaaaa Ed Waziri Gwajima atoa siku 10 sakata mgonjwa aliyefumuliwa nyuzi

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

TUKIO la tabibu wa Zahanati wa Kerenge, Kata ya Kibaoni, wilayani Korogwe, kudaiwa kumfumua nyuzi majeruhi wa ajali ya pikipiki limemwibua Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ambaye ametoa maagizo kuhusu tukio hilo.

Tabibu huyo, Jackson Meli, anayetuhumiwa kumfumua nyuzi majeruhi, Zubeda Ngereza aliyapata ajali ya pikipiki Julai 28, mwaka huu na kupelekwa katika zahanati hiyo, kushindwa kulipa gharama ya matibabu Sh. 10,000.

Tukilo hilo ambalo video yake ilisambaa katika mitandao ya kijamii juzi ilizua gumzo na maswali kadhaa juu ya undani wa tabibu huyo kudiriki kuchukua uamuzi huo.

Video hiyo ilimwonyesha tabibu huyo akikiri kufanya tukio hilo mbele ya Diwani wa Kata ya Kerege, Abdallah Robo, aliyekuwa akimhoji. Akieleza kwamba alitaka kulipwa gharama za matibabu.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Wizara hiyo jana, ilimnukuu Waziri Gwajima akitoa agizo kwa mabaraza yote ya kitaalamu yanayohusika na usimamizi wa huduma za afya nchini yafike katika Halmashauri ya Korogwe kuchunguza tukio hilo, kuchambua mfumo mzima wa utoaji huduma kwa wagonjwa, ili kubaini hali halisi na kupanga hatua stahiki.

Kupitia taarifa hiyo, Waziri Gwajima alisema: “Mabaraza yote ya kitaalamu yanayohusika na usimamizi wa huduma za afya nchini yanapaswa kwenda kuchunguza tukio hilo ili kubaini hali halisi na kupanga hatua stahiki za kuchukua kuhusu sakata hilo”.

Mbali na kueleza hayo, Dk. Gwajima pia alitoa siku 10 taarifa ya tukio hilo iwe imekamilika na kuwasilishwa mezani kwake.

Akizungumza na Nipashe juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Halfani Magani, alikiri kuwapo kwa tukio hilo, kwamba tabibu huyo alishaondolewa katika zahanati hiyo, aliwapokea majeruhi hao na kuwapa huduma.

Alisema halmashauri hiyo ilipokea taarifa hizo na kwa kushirikiana na polisi walimkamata tabibu huyo ambaye alikaa chini ya uangalizi katika Kituo cha Polisi Korogwe kuanzia Julai 28 hadi 30, mwaka huu, kisha alisimamishwa kazi na kumpatia hati ya mashtaka kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa umma.

Magani alisema huduma ambazo aliwapatia zilikuwa pamoja na kumshona mama huyo nyuzi katika eneo la mkono na kumfunga bandeji na dereva wa bodaboda alifungwa bandeji maeneo aliyoumia.

Kwa mujibu wa Magani, baada ya huduma hiyo ndipo tabibu alipodai gharama za matibabu ambazo kwa huyo mama zilikuwa ni Sh. 10,000 na aliposhindwa kulipa kwa wakati huo, akafanya uamuzi wa kumfumua nyuzi.

Chanzo: ippmedia.com