Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema wakati umefika kwa jamii kuacha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto na badala yake kusimamia misingi ya upatikanaji wa haki.
Amesema hayo akiwa Wilayani Tarime Mkoani Mara, alipotembelea kituo cha Nyumba Salama cha Masanga kinachotumika kuwalea watoto waliokumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au walio katika hatari ya kukumbwa na vitendo hivyo.
“Jamii lazima ishiriki kikamilifu kufuatilia matatizo yanayowakumba wanajamii husika na kama wanashindwa kufanya hivyo wanakuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo”
Aliongeza kuwa, katika baadhi ya maeneo nchini watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili na kukoseshwa haki ya elimu ilhali watumishi wanaopaswa kuingilia kati suala hilo wanabaki kimya na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji katika ngazi mbalimbali wanabweteka na kulipwa mshahara bila kuufanyia kazi.