Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazijua njia sahihi za kupiga mswaki?

53139 Pic+mswaki

Fri, 19 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hivi unajua kwamba watu wengi hawafahamu kanuni au njia sahihi za kupiga mswaki (kusafisha kinywa) kwa umakini?

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kinywa kikiwa safi huzuia magonjwa ya fizi na kutoboka kwa meno lakini changamoto iliyopo kwa baadhi ya watu ni namna ya kusafisha fizi, meno na ulimi kwa ufasaha.

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa afya ya kinywa na meno kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila (Mamc), Cecilia Kayombo alisema watu wengi hawajui kupiga mswaki kwa usahihi.

Alisema ili kufanikisha usafi wa kinywa na meno, kila mtu anapaswa kuzingatia upigaji sahihi wa mswaki siku zote au inapohitajika.

Dk Kayombo alisema kinywa safi ni msingi wa afya bora na pia huzuia magonjwa ya fizi na kutoboka kwa meno. “Ili kutunza afya ya kinywa na meno, lazima uhakikishe unapiga mswaki kwa ufasaha, kwanza inatakiwa brashi zake (za mswaki) ziwe zimenyooka. Kwa mfano, ufagio ukiwa umekwisha hauwezi kufagia vizuri, vivyo hivyo hata katika mswaki,” alisema Dk Kayombo.

“Kichwa cha mswaki kinatakiwa kiwe na duara kabla ya brashi zinapoanzia mbele ya mswaki ili kuwe na uwiano mzuri, yaani kama mkonga fulani mbele ili kuweze kupiga mpaka kwenye meno ya mwisho kabisa bila kuumia wala mkono kuchoka.”

Kuhusu hatua za kuzingatia katika upigaji mswaki, Dk Kayombo alisema, meno yana sehemu tatu ambazo ni nje, ndani na pa kutafunia, lakini kuna taya mbili juu na chini na upande wa kulia na kushoto.

“Sehemu zote lazima zisafishwe, wewe mwenyewe unaamua unaanzia wapi. Kwa mfano, mimi natumia mkono wa kulia kwa hiyo naanzia taya la juu kulia upande wa nje kwa njia ya kuzungusha mswaki naenda juu chini na baadaye nasawazisha,” alisema daktari huyo.

“Kumbuka hakuna njia nzuri kuliko nyingine, unasafisha upande wa nje unamaliza unaingia upande wa ndani na unahamia kushoto baadaye unahama upande wa nje chini kwenda juu ulipoishia… ukipeleka ulimi wako utaona pako sawa,” alisema Dk Kayombo.

Mmoja wa watu ambao wamekumbana na changamoto hiyo ya kupigwa mswaki ni Naomi Athanas, mkazi wa Kimara Bonyokwa, Dar es Salaam ambaye, alisema juzi kuwa, “ninapiga mswaki muda mrefu, lakini sijui kwa nini huwa siufikii uchafu wote uliopo mdomoni (kinywani) mwangu, hali hii hunikera hasa sehemu ya ndani ya meno,” alisema Naomi.



Chanzo: mwananchi.co.tz