HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imepongezwa kwa kuwapa uhakika wa matibabu wazee wilayani hapa kwa kuwapa vitambulisho maalumu kwa ajili ya kupata tiba bure kwenye vituo vya huduma ya afya.
Kwa mujibu Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Mbarali, Hezron Kapwela, asilimia kubwa ya wazee wilayani hapa sasa wanapata matibabu bure baada ya halmashauri kupitia ofisi ya mganga mkuu wilaya kuratibu kwa ufasaha wa kutoa vitambulisho na kadi za CHF kwa wazee.
Kapwela alisema hatua iliyofikiwa na serikali kuwapa wazee vitambulisho kwa ajili ya kupata matibabu bure ni jambo linalowapa faraja kwa kiasi kikubwa.
Alisema wengi wao sasa wanao uhakika wa kupata matibabu tofauti na awali licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kwenye baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za afya.
Hata hivyo aliomba wazee wanapofika kwenye vituo vya matibabu wakiwa wamesahau kadi zao waweze kupokelewa na kutibiwa, akisema mara nyingi hutokea kwa bahati mbaya hasa kwa kuwa umri wa uzee huambatana na kusahau.
Baraza hilo pia liliipongeza halmashauri kwa kuimarisha mabaraza ya wazee katika ngazi ya kata na vijiji ambapo sasa kata zote 20 mabaraza yameundwa na yako imara.
Alisema Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kupitia Idara ya Ustawi wa jamii imefanya kazi kubwa kuimarisha mabaraza ya wazee, jambo linalowapa moyoa na kuona serikali inawajali.
Kapwela aliyataja mabaraza ya wazee kuwa muhimu katika ustawi wa watu wa kundi hilo kwa kuwa ndiyo yaliyo na jukumu la kutetea na kufuatilia haki zao sambamba na kuishauri jamii juu ya nini wazee wanahitaji baada ya kulitumikia taifa lao kwa miaka ya ujana wao.
Katibu huyo pia alishauri kuwepo na mikopo itakayotolewa na halmashauri kwa wazee ili kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha ujasiriamali na kujikomboa kiuchumi.
Alisema vipo vikundi vya wanawake wazee wanaojishughulisha na shughuli ndogondogo ambao iwapo wangewezeshwa kupitia mikopo ya halmashauri au wadau wengine wanaoweza kuwakopesha pasipo riba na wao wangeondokana na utegemezi kama ilivyo kwa wanawake,walemavu na vijana wanaogawana asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri kupitia kukopeshwa.
Kwa upande wake, Ofisa Ufuatiliaji wa Shirika la Kiwwauta, Mussa Mcharo alisema ili kuboresha zaidi huduma ya matibabu kwa wazee ni muhimu wakapewa vitambulisho vyenye kuwawezesha kupata kadi katika halmashauri zote nchini kwakuwa kwa sasa wanapata tabu pale wanapougua wakiwa safarini.