Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi watakiwa kuondoka na uchafu baada ya kujifungua

22460 WAZAZI+PIC TanzaniaWeb

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Changamoto katika sekta ya afya haziishi kwenye uchache wa madaktari, wahudumu wa afya, majengo na umbali katkati ya vituo vya afya na makazi ya wananchi, bali pia suala la vifaa tiba na miundombinu mingine.

Ndivyo ilivyo pia katika kijiji na kata ya Bwambo wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, ambako wazazi wanatakiwa kuondoka na uchafu ikiwemo kondo la nyuma baada ya kujifungua.

Hatua hiyo inatokana na zahanati ya kijiji hicho kutokuwa na vifaa vya kuhifadhia taka ngumu. Hata hivyo, mganga mkuu wa Wilaya ya Same, Dk Godfrey Andrew aliliambia Mwananchi mwishoni mwa wiki kuwa, hana taarifa juu ya uwepo wa changamoto hiyo huku akiahidi kufuatilia kujua ukweli na kuwataka wananchi kushiriki katika ujenzi wa zahanati na siyo kuitegemea Serikali.

“Ukisema Serikali itajenga zahanati zote huo ni uongo. Wakati mwingine wananchi wanatakiwa kuelekeza nguvu zao wenyewe katika kuhakikisha wanasaidiana na Serikali,” alisema Dk Andrew wakati akifafanua juu ya uhaba wa changamoto ya miundombinu katika zahanati na vituo ya afya.

Wakazi wa eneo hilo wanasema kwa muda mrefu wamelalamikia jambo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Wanasema mbali na kutakiwa kuondoka na uchafu, zahanati hiyo inayohudumia zaidi ya wakazi 5,000 pia haina choo, bafu wala maji kwa ajili ya wazazi baada ya kujifungua. Mkazi wa kijiji hicho, Janeth Mdee alisema tatizo hilo limedumu muda mrefu na imekuwa ni kawaida kwa wanawake kuondoka na uchafu baada ya kuruhusiwa kurejea majumbani mwao. “Tunaomba jambo hili litazamwe kwa macho mawili maana hakuna maji, choo, bafu wala sehemu ya kuchomea taka. Kwa kweli tunapata tabu,” alisema Janeth.

Robson Jones alisema wazazi wanadhalilika wanapokwenda kujifungua kutokana na kukosa maji na huduma muhimu.

“Tunamuomba waziri wa Afya atusaidie jambo hili kwani tumechoka wake zetu kudhalilishwa, yaani mwanamke kubebeshwa kondo la nyuma wakati akishajifungua, hii ni aibu kubwa kwa jamii yetu,” alisema.

Muuguzi wa zahanati hiyo, Merrystella Msuya alisema matatizo hayo ni ya muda mrefu na kwamba wamekuwa wakijisikia vibaya kuwataka wazazi kuondoka na uchafu baada ya kujifungua. “Zahanati hii haina choo wala maji, kwa hiyo akinamama wakijifungua hapa inatulazimu tuwaambie wabebe taka zao wapeleke nyumbani, nadhani hii sio sahihi,” alisema Merrystella.

“Tunaomba Serikali itusaidie au watuambie kama wameshindwa kutekeleza hili jambo la kuhakikisha vyoo vinakuwepo pamoja na maji.”

Muuguzi mkunga wa zahanati hiyo, Daudi Christopher alisema chumba cha kuwapumzisha wagonjwa na wodi za wazazi kutokuwa na maji ni miongoni mwa changamoto zinazowatesa.

Mbunge wa Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka alisikitishwa na baadhi ya watendaji kukwamisha maendeleo ya wananchi na wengine kutokuwa waaminifu licha ya fedha za kata kupitia mfuko wa jimbo kutolewa.

Chanzo: mwananchi.co.tz