Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi watakiwa kuchunguza watoto wao saratani ya macho

15e25b020abb420b35e45ffed324fccb Wazazi watakiwa kuchunguza watoto wao saratani ya macho

Mon, 7 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Saratani ya macho kwa watoto imeelezwa kuwa tishio huku wazazi wakitakiwa kuwa makini kukagua watoto wao.

Dalili kubwa imeelezwa kwamba ni jicho kuwaka kwa ndani na kisha kuonekana kama lina kengeza.

Meneja wa Programu ya Macho kutoka Wizara ya Afya, Bernadetha Shillo alisema hayo juzi wakati wa semina kwa waandishi wa habari iliyotanguliwa na maadhimisho ya Siku ya Satarani Duniani.

Alisema saratani ya macho kwa watoto imekuwa ni tishio huku watoto wengine wakizaliwa wakiwa na saratani hiyo.

Alisema saratani hiyo imekuwa ikiathiri zaidi watoto wa miaka mitatu hadi mitano na kwamba umri wa mtoto unavyoendelea kuwa mkubwa inaweza kutoka jicho moja hadi kuathiri lingine.

"Saratani hii hutokana na hitilafu inayotokea kwenye vinasaba ambayo huathiri utando wa fahamu wa jicho na huanza kujitokeza baada ya miaka mitatu tangu mtoto alipozaliwa," alisema.

Alisema ni mara chache sana hujitokeza baada ya miaka mitano.

Alisema saratani hiyo huwapata watoto wa jinsi zote kwani inahusisha vinasaba na hivyo inarithiwa.

"Saratani ya macho huwa iko ndani sio rahisi uione, dalili kubwa inayoonekana ni jicho kuwaka kwa ndani. Saratani inavyoendelea kukua jicho linakuwa na kengeza na inaendelea kuathiri pembeni ya jicho," alisema.

Alisema ukuta wa jicho unapopasuka jicho linavimba, linaathiri hadi kwenye mifupa na hata huweza kumfanya mtoto kupoteza maisha.

Alisema kwa mtoto ambaye alichelewa kupata matibabu jicho huwa linaondolewa na kwamba kama mtoto atawahishwa kwenye matibabu atapewa mionzi na dawa.

Aliwashauri wazazi kuwafikisha watoto mapema hospitali pindi wanapoona dalili za saratani ya macho.

Siku ya Saratani Duniani huadhimishwa kila mwaka Februari 4. Siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 2000 mjini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa dunia wa saratani na ni maalumu ili kutoa elimu ya kinga na kuelimisha wananchi na serikali hatua za kuchukua katika kukabiliana na ugonjwa huu.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani kwa mwaka 2022 ni ‘Huduma za saratani sawa kwa wote.’

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema ujumbe unalenga kila mtu awajibike kushiriki katika kupambana na saratani.

Pia kila mtu kupima afya yake, kujikinga na vyote vinavyoweza kusababisha saratani, kusaidia wagonjwa wa saratani na kuwa na hospitali zinazoweza kutoa huduma ya saratani ili kupunguza janga la ugonjwa huo na athari zake zake.

Waziri alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz