Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wanavyoona aibu kuzungumza na watoto kuhusu uzazi wa mpango

55323 Wazazi+pic

Fri, 3 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Umewahi kufikiria kumweleza mtoto wako wa miaka sita na kuendelea kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango na athari za uzazi usio salama?

Wengi mtasema hamjawahi kwa sababu mnawaoenea aibu kutokana na umri wao mdogo, na kuwaza hawapaswi kuelezwa mambo hayo.

Aibu ya wazazi ni chanzo cha watoto na vijana kukosa elimu sahihi inayohusu uzazi usio salama ikiwamo utoaji wa mimba kwa njia zisizo sahihi.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi katika mahojiano maalumu Kijiji cha Nyalikunga A wilayani Magu Mkoa wa Mwanza, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Geita, Mathew kazimoto anasema wazazi hawana muda wa kuzungumza na vijana pamoja na watoto wao.

Pia, anasema hawajui ya kuwa elimu kuhusu afya ya uzazi ni muhimu sana katika makuzi ya vijana.

“Wazazi wengi hawana muda, wengi wanaona aibu kwa kudhani kuwa wanawaruhusu vijana wao kwenda kufanya tendo la ngono,”anasema Kazimoto ambaye pia ni katibu wa Kanisa la Sabato Magu.

Mwalimu Kazimoto anasema aibu ya wazazi kutoweza kuwapa watoto wao elimu ya makuzi na afya ya uzazi imesababisha mabinti wengi kutoa mimba kwa kutumia vidonge.

“Huku kwetu vijana wa kike hutumia vidonge kutoa mimba kwa sababu huvipata kwa urahisi katika maduka ya madawa, na wapo wengine ambao katika hekaheka za utoaji wa mimba kwa hivyo vidonge hupoteza maisha,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa kidemografia na afya (DHS) za mwaka 2015/16 katika kila vizazi hai 100,000, wanawake 556 hufariki dunia kutokana na matatizo mbalimbali ikiwamo kutohudhuria kliniki, lishe duni, kifafa cha mimba, kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua, uchungu wa muda mrefu na utoaji wa mimba usio salama.

Pia, ripoti za waratibu wa afya ya uzazi na mtoto wa mikoa, Mwanza inaeleza kuwapo vifo 151 kuanzia Januari hadi Desemba 2018, chanzo kikiwa ni ukosefu wa elimu ya uzazi kwa vijana.

Wanachosema wazazi

Rosemary Mhikwa 56, ni mama wa watoto saba, anasema anashangaa ni nini kimewapata wazazi wa leo kwa sababu sasa hivi kumkanya mtoto wa mtu ni kutafuta ugomvi.

Anasema zamani mzazi alikuwa na uwezo wa kukanya mtoto wa mzazi mwingine bila tatizo lolote lakini siku hizi mzazi au mtu mzima yeyote anaweza kuona mtoto anafanya ujinga na asimwambie kitu kwa kuogopa kugombana na mzazi wa mtoto husika.

“Kipindi chetu tulikuwa tukikanywa na mzazi yeyote yule haijalishi kuwa hajakuzaa na tulisikiliza tofauti na sasa. Wazazi hawaongei wakiona vijana wanapotoka na hapa ndipo panaposababisha mabinti zetu kushika ujauzito katika kipindi ambacho hawazihitaji na mwisho wa siku kulazimika kutoa kabla hawajagundulika na wazazi wao, na kujikuta wakitoa katika njia zisizo salama,” anasema Mhikwa.

Hoja hiyo inaungwa na mzazi Elias Makelele akisema aibu ni chanzo kikubwa kinachosababisha vijana wengi kukosa elimu ya makuzi.

“Kuna tatizo la ukaribu na kutokuwa wazi kati ya wazazi na vijana wao. Wazazi hawana uwezo wa kuongea masuala haya ya makuzi wanaona haya. Labda kuwe na semina nyingi, wataalamu wa afya watusaidie kwa kuleta semina mbalimbali zinazohusu afya na makuzi kwa vijana wetu,” anasema Makelele.

“Mikutano kuhusu afya ya uzazi haipo siku hizi. Kupitia mikutano hiyo jamii ilikuwa ikipata elimu ya kutosha na hata wazazi ambao hawana uelewa kuhusu masuala haya alikuwa akijifunza na baadae kwenda kufundisha watoto wake.

“Vijana wana maswali magumu na kiukweli wakati mwingine ni vigumu mimi kuongea na kijana wangu ila kupitia mikutano na semina za aina hiyo; vijana walikuwa wakipata nafasi ya kuuliza maswali yao yanayowatatiza.”

Anaomba jamii ibadilike kwa kuvua aibu zao na kuwaelimisha vijana wao.

Wataalamu wa afya wanasemaje?

Muhudumu wa Afya, Kata ya Magu Juliana Mathias anasema pamoja na kupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu za afya, amegundua wazazi wengi ni wakali mno na hawana ukaribu kabisa na vijana wao.

“Badala ya mzazi kukaa na kuzungumza na mtoto wake pale tatizo linapotokea mfano kupata mimba; mama anajiuliza ataanzaje kumshirikisha baba wa binti na mwisho wa siku mama na mwanae wanajikuta wakishirikiana kutoa mimba kwa njia zisizo rasmi,” anaongeza.

Sheria ya kanuni ya adhabu kifungu namba 150, inakataza mtu yeyote kuharibu mimba iwe mwanamke huyo ana mtoto au hana, kinyume cha sheria akamlisha au akamfanya ale sumu au kitu kingine cha kudhuru mimba, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka kumi na nne kusababisha kuharibika mimba.

Na kifungu 152 kinasema kuwa mtu yeyote ambaye anatoa au anampa mtu yeyote kitu chochote, akijua kwamba kinakusudiwa kutumika kinyume cha sheria kumfanya mwanamke aharibu mimba, iwe mwanamke huyo ana mtoto au hana, atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu .

Shinje Shinyanga 20, amemaliza kidato cha nne anasema katika makuzi yake hakuwai kuelezwa masuala ya afya ya uzazi bali alijifunza mwenyewe kupitia makundi shuleni.

“Kutokana na kutokuwa na elimu sahihi, mabinti hutoa mimba kwa kutumia soda, majivu na majani ya chai. Mimi mwenyewe kuna kipindi niliwahi mdanganya rafiki yangu wa kiume kwamba nimepata mimba, alichofanya ni kwenda dukani akaniletea misoprosto minne na akaniambia ninywe miwili na mingine niweke ukeni.

“Huyo alikuwa ana uwezo wa kuzinunua kwa Sh 40,000 vipi kwa wale ambao hawana uwezo hawa ndiyo uishia kutumia njia zisizo sahihi,”anasema Shinje huku akitabasamu

“Natamani wazazi wangu wangekuwa wazi kwangu, bado nina maswali mengi sana ila wazazi hawatupi nafasi ya kujifunza kutoka kwao, mfano mimi mzazi wangu ni mkali na pia naona kama anaona haya na anaona kuongea na mimi kuhusu jinsi ya kujilinda ni kama ananituma,”anasema.

Roman Kiwango, muangalizi wa magonjwa majumbani anasema uwapo wa makundi rika kipindi cha nyuma yalikuwa yakisaidia kutoa elimu kwa vijana hasa wanafunzi.

Emanuel Musa (22) anasema hakuwahi kupewa elimu, yeye anasema, “Mimi nilijifunza kupitia wenzangu, kifupi jamii yetu haina elimu kabisa. Elimu sahihi itolewe, wengi wetu hujifunza mambo katika vijiwe,” anasema Emanel ambaye ni dereva bodaboda.

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto Kifungu 32 unasema, Haki ijulikane kwa wote; Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa wazazi na watoto wanafahamu vizuri sheria hii ili waitekeleze vyema. Pia, watoto wafundishwe kuhusu haki zao.

Mkataba wa haki za watoto wa mwaka 1989 unasisitiza kumshirikisha mtoto katika kila jambo linalomuhusu.

Hivyo ni haki ya kijana au mtoto kupata elimu ya makuzi na afya. Hii itamjengea kuwa kijana makini zaidi katika jamii inayomzunguka.

Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inashughulikia haki za watoto Tanzania. Sheria hii inajumuisha mambo mbalimbali ikiwamo kutetea masuala yote ya kuboresha, kulinda na kuhifadhi ustawi wa mtoto pamoja na haki zake.

Sheria hii inafafanua kuwa mtoto ana haki ya kupata huduma bora za elimu, malazi na matibabu kwa ajili ya ustawi wake na wakati huo huo mzazi au mlezi ana wajibu wa kumtunza mtoto pamoja na kumpa elimu na malezi bora.



Chanzo: mwananchi.co.tz