Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauza tangawizi, malimao, ukwaju wasimulia corona ilivyowanufaisha

Ad4d9d09e73491c3784123e7705d14a4 Wauza tangawizi, malimao, ukwaju wasimulia corona ilivyowanufaisha

Wed, 11 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYABIASHARA wa tangawizi, mchaichai, malimao, pilipili na ukwaju, wamesema homa ya virusi vya corona, ilileta neema kwao licha ya watu kujifungia ndani kwa hofu ya kuambukizwa.

Mfanyabiashara wa tangawizi na ukwaju katika Soko la Kilombero mkoani Arusha, Emmanuel Mollel alieleza jana kuwa bidhaa hizo, zilitumika kwa wingi kuongeza kinga ya mwili na kama tiba ya homa hiyo.

Mollel alieleza kuwa kuwa janga hilo la corona, limegeuka kuwa baraka kwake kwani ameweza kujenga nyumba.

"Nilikuwa nauza gunia la kilo 160 la tangawizi kwa muda wa siku mbili na ukwaju nilikuwa nauza mpaka kilo 30 kwa siku na kilo moja ni shilingi 3,000, niliweza kujenga nyumba kwa kipindi cha miezi miwili," alisema Mollel.

Alisema "Siwezi kukuambia nilikuwa napata kiasi gani kwa siku. Lakini hivi sasa hali imekuwa tofauti, kwani naweza kusota na gunia moja zaidi ya wiki mbili".

Mfanyabiashara wa malimao, Pendo Akyoo alisema anajivunia kununua pikipiki aliyomkodishia mtu, ambayo inamsaidia kukidhi mahitaji yake. Alisema biashara yake ilikuwa nzuri kipindi cha corona, lakini kwa sasa biashara hiyo imedorora.

"Biashara ya malimao hivi sasa imeshuka ukilinganisha na kipindi cha corona. Nawaomba watanzania waendelee kutumia bidhaa hii. Tuliambiwa malimao yanaongeza kinga ya mwili, hivyo tutambue kuna magonjwa mengi zaidi ya corona yanayotibiwa na corona," alibainisha.

Amina Rashid ambaye ni muuzaji maarufu wa mchaichai, alisema mtaji wake ulipanda kutoka Sh 20,000 hadi Sh 200,000 kutokana na biashara hiyo wakati wa corona. Pia alisema kutokana na bishara ya mchaichai, amepata fedha ya kutosha kulipia ada watoto wake wanaosoma shule binafsi.

"Nilikuwa nauza mchaichai hadi shilingi 50,000 kwa siku. Tangu nianze kuuza biashara hii, sijawahi kupata fedha nyingi kama wakati wa corona na niliweka akiba ya kutosha," alifafanua.

Alisema wakati wa corona alikuwa akitembea porini kutafuta bidhaa hiyo, iliyosakwa na wengi kama lulu, kwa ajili ya kunywa na kujifukiza.

Lakini, alisema hivi sasa bidhaa hiyo haina soko na inapoteza harufu yake sokoni kwa kukauka.

Chanzo: habarileo.co.tz