Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauguzi wadaiwa kusababisha kifo cha mjamzito, DC atoa saa 72

34125 Mjamzito+pic Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo ametoa siku tatu kwa uongozi wa Hospitali ya Wilaya Igunga kuchukua hatua dhidi ya wauguzi wawili wanaodaiwa kusababisha kifo cha Milo Peter na mwanaye mchanga.

Amechukua uamuzi huo jana Desemba 29, 2018 baada ya kupata taarifa za tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Desemba 28, 2018 kutoka kwa wajawazito waliokuwa katika hospitali hiyo, walioshuhudia kitendo hicho kinachodaiwa kuwa ni uzembe.

Milo, mkazi wa mtaa wa Masanga Igunga mjini alikwenda katika hospitali hiyo Desemba 27, 2018 kwa ajili ya kujifungua.

Jana, ndugu wa marehemu waligoma kuchukua mwili  wa Milo wakitaka ufanyiwe uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.

Wakati wakiandamana kuelekea kwa Mwaipopo walikutana na diwani wa Igunga mjini (CCM), Charles Bomani na kuwashauri wakazungumze kwanza na uongozi wa hospitali hiyo.

Baadhi ya wajawazito waliolazwa wodi ya wazazi katika hospitali hiyo wamedai kuwa watumishi hao walizembea  na kusababisha kifo cha mama huyo na kichanga chake.

Kutokana na kuwakosa watuhumiwa hao kuthibitisha tuhuma zinazowakabili, Mwananchi halijawataja majina.

Wanawake hao wakizungumza na Mwaipopo ambaye pia alikutana na uongozi wa hospitali hiyo, wameeleza kuwa marehemu hakupewa msaada na wauguzi hao licha ya kuomba msaada kutoka kwa wauguzi wa zamu.

“Pamoja na kuomba msaada hakupewa na kuna mhudumu mmoja alikuwa anahangaika na simu yake tu muda wote,” amesema Blandina Enock.

Akinamama hao wamemueleza diwani huyo kuwa baada ya marehemu kupatiwa kitanda ndugu zake waliruhusiwa kurejea nyumbani lakini baadaye alishikwa na uchungu na kuomba msaada huo wa wauguzi bila mafanikio.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Igunga, Amada Kasigwa amesema marehemu na kichanga kilichokuwa na kilo 3.8 walifariki dunia Desemba 28 saa 9 alfajiri.

Alidai kuwa mmoja wa wauguzi aliyekuwa zamu ni mzembe (anamtaja jina) na kubainisha kuwa amewahi kuonywa mara kadhaa, hasa tabia yake ya kuomba rushwa wagonjwa.

Mwaipopo ametoa maagizo hayo baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na uongozi wa hospitali hiyo.

"Nasubiri muda niliowapa ukimalizika ndio nione hatua ya kufanya,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz