Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauguzi Dar, Dodoma wapigwa msasa kwa siku nne

Wauguzi Pic Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan(AKU), Dk Eunice Pallangyo

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Wauguzi wa hospitali na vituo vya afya jijini hapa na Dodoma, wamepatiwa mafunzo ya fani hiyo ili nao wawafundishe vema kwa vitendo wanafunzi wa shahada ya kwanza.

Mafunzo hayo ya siku nne yaliyotolewa na Shule ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), yamehitimishwa jana.

Wakunga na wauguzi hao wanatoka katika vituo vya afya na hospitali ambazo wanafunzi wa shahada ya kwanza ya uuguzi watakwenda kupata mafunzo kwa vitendo.

Mafunzo hayo yamekuja wakati AKU inajiandaa na programu mpya ya kuwadahili wanafunzi wa shahada ya kwanza ya uuguzi wanaohitimu masomo ya kidato cha sita na watasoma kwa miaka minne.

Awali, AKU ilikuwa ikidahili wanafunzi waliokuwa na elimu ya stashahada na uuguzi na ukunga waliokuwa wakifanya kazi katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Julai 21, 2023 Mkuu wa AKU, Dk Eunice Pallangyo amesema mafunzo hayo yalianza Jumatatu na kuhitimishwa jana Alhamisi Julai 20, 2023.

Dk Pallangyo amesema kozi hiyo itaanza Novemba mwaka huu.

“Tunataka tuwapike wanafunzi hawa kwa viwango vya juu, sasa ili ufanikiwe lazima ufanye maandalizi ikiwamo kuandaa walimu wa viwango jambo ambalo tumeshalifanya.

“Walimu hawawezi kufanya kazi pekee yao hasa katika taalumu hii ya uuguzi inayohitaji ujuzi na maarifa makubwa ya kukaa na wagonjwa wa aina mbalimbali,” amesema Dk Pallangyo.

Dk Pallangyo amesema elimu haina mwisho wameamua kuwaita wauguzi hao ili kuwajengea uwezo zaidi.

“Tunataka wote tuongee lugha moja, wanafunzi wetu wakitoka chuoni kwenda kwao wasipate shida katika mafunzo yao ya vitendo. Kwa maana nyingine, mafunzo haya yanawaandaa wasimamizi na washauri watakaowaongoza wanafunzi kuhusu fani ya uuguzi.

“Miaka minne ni safari ndefu, ndio maana tunaimarisha uhusiano wetu na wadau hawa tunaowajengea uwezo. Huu ni mwanzo tu, hatutaishia hapa tutakuwa tukiwajengea uwezo mara kwa mara,” amesema Dk Pallangyo.

Mratibu wa Maabara za Sayansi na Mafunzo kwa Vitendo wa AKU, Kisimbi Mressa amesema jumla ya wauguzi 15 kutoka hospitali za Mwanyamala, Mbagala Rangitatu, Amana, Temeke, Muhimbili na Milembe mkoani Dodoma wameshiriki mafunzo hayo ya siku nne.

Mressa amesema kozi hiyo pia imeshirikisha wakunga na waaguzi wabobezi wa hospitali hizo, akisema wamewajengea uwezo katika mada za kukabiliana na migogoro mbalimbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Kama unavyojua mgonjwa anatarajia atahudumiwa kwa kiwango fulani ikiwa kinyume ndipo mgogoro unaanza. Tumewafundisha namna ya kuwaelekeza wanafunzi jinsi ya kukabiliana au kutatua migogoro itakayojitokeza,” amesema Mressa.

“Tumewafundisha namna ya kuwajengea ujasiri wanafunzi wa kukabiliana na hali tofauti za mshtuko. Kuna siku mwanafunzi anaweza akamuona mgonjwa wodini amepasuka kichwa, hali itakayompa mashtuko utakaomsababisha kuichukia fani yake.”

Mmoja wa wauguzi wa Hospitali ya Aga Khan waliohudhuria mafunzo hayo, Goodluck Marandu ameishukuru AKU akisema walichofundishwa ni vitu ambavyo kila siku wanakumbana navyo katika utekelezaji wa majukumu yao

Chanzo: Mwananchi