Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi 5 afya wasimamishwa kupisha uchunguzi

F6081d72755a3d8a01e1ce10ee1788f9 Watumishi 5 afya wasimamishwa kupisha uchunguzi

Wed, 20 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATUMISHI watano kati ya sita wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio Ukerewe wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa vyombo vya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mabaraza na bodi za kitaaluma.

Watumishi hao tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani zaidi ya Sh Milioni 200 na mmoja wao alikiri na kuhukumiwa kulipa Sh milioni 100 na waliobaki walirejeshwa kazini.

Hata hivyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima hivi karibuni aliagiza watumishi hao kusimamishwa kazi kufuatia Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe kudai kuwa hakuridhishwa na watumishi hao kurejeshwa kazini kwani hawaaminiki tena kwenye utumishi wa umma na kamwe haiwezekani na haieleweki inawezekanaje mtumishi wa umma aibe halafu akishalipa anarejeshwa kazini.

Katika taarifa ya Wizara ya Afya, inasema kuwa hata hivyo Dk Gwajima alipotembelea hospitali hiyo ya Nansio alijionea viashiria vya udanganyifu katika mfumo mzima wa ugavi wa dawa hivyo kukubaliana na maelezo ya Mkuu wa Wilaya kuwa bado kuna tatizo kama alivyoeleza.

Kufuatia hali hiyo, alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ukerewe . Esther Chaula kuwasimamisha kazi watumishi hao na kuwafikisha kwenye kamati ya maadili ya utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma na vyama vyao ili waone kama kweli hao watumishi bado wanastahili kuaminika tena kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma pia maadili ya vyama vyao vya kitaaluma.

“Mahakama imefanya maamuzi kwa mujibu wa sheria wakalipa, hata hivyo naagiza Mkurugenzi kama tulivyokubaliana uendelee kusimamia hatua za kinidhamu na kiutumishi pia uwafikishe kwenye mabaraza na bodi zao za taaluma pamoja na vyama vyao vya taaluma ili nao wawachunguze na kuwachukulia hatua,” aliagiza Dk Gwajima.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk Thomas Rutachunzibwa watumishi hao wameshasimamishwa kazi na hatua zaidi za kinidhamu, maadili na kiutumishi zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao.

Chanzo: habarileo.co.tz