Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu wenye Ualbino waituhumu sekta binafsi kuwabagua

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya waajiri wa sekta binafsi wamedaiwa kuendeleza ubaguzi wa kutowaajiri watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wakiamini  wana mkosi.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Novemba 27, 2018 na Mkurugenzi wa Shirika la Under the Same Sun, Berthasia Ladislaus wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wahitimu 15 wenye ualbino wa ngazi mbalimbali.

Amesema watu wenye ualbino bado wanakabiliwa na ukosefu wa ajira kutokana na waajiri wengi kuwabagua hasa sekta binafsi jambo ambalo ni kinyume na sera ya Serikali ya mwaka 2009 inayotaka kila mwajiri kuhakikisha anatoa  asilimia tatu ya ajira kwa watu wenye ulemavu.

"Changamoto ya ajira ni kubwa kwa watu wenye ualbino jambo linaloathiri hata  programu yetu ya ufadhili wa masomo kwa watu wenye ualbino.

“Bado wengi wanabaguliwa katika fursa za ajira  na kujiajiri hasa sekta binafsi kutokana na dhana potofu ikiwamo ualbino ni mkosi," amesema.

Amesema waajiri hao mbali na kuona ualbino ni laana na mkosi bado wana amìni kuwaajiri albino wanaweza kuwaambukiza waajiri au wafanyakazi wenzao na wateja  wao mikosi hiyo.

"Tunaiomba Serikali ije na mkakati utakaokuwa tiba kwa tatizo hili la kibaguzi, hususani kusimamia utekelezaji wa sheria namba 9 yà mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda," amesema. 

Kuwa upande wake, mshauri wa wanafunzi wenye ualbino katika masuala ya ajira , Josephat Igembe amesema  suala la albino kubaguliwa na waajiri wa sekta binafsi ni kubwa kwani hata baadhi ya waajiri wa sekta hiyo  wanapoitwa kwenye vikao vya kuwaelimisha wengi wao wamekuwa hawafiki.



Chanzo: mwananchi.co.tz