Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu watano huambukizwa VVU kila siku

Chanjo Ukimwi Pic Data Watu watano huambukizwa VVU kila siku

Fri, 2 Sep 2022 Chanzo: mwanachidigital

Watu watano wanakadiriwa kupata maambukizi mpya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa siku hasa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Wilaya ya Kongwa.

Hali hiyo inaonekana kutokana na mwingiliano wa watu kuwa mkubwa na kukosa elimu sahihi ya kujikinga na maambukizi ya VVU.

Akizungumza wakati akikabidhi Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema makadirio ya wastani wa maambukizo mapya kwa mwaka huu ni takribani watu 1999 kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49.

Alisema kati ya idadi hiyo, wanawake ni 1,161 na wanaume 838.

Alisema wastani wa watu 52,842 wanahisiwa wanaishi na maambukizi ya VVU Mkoa wa Dodoma hadi kufikia Juni 2022, huku wanawake wakiwa 30,264 na wanaume 16,476.

Rosemary alisema hali ya wahisiwa wanaoishi na VVU inaonekana kushamiri zaidi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Wilaya Kongwa.

Mratibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Erico Kawanga alizitaja miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU ni kutoa elimu kwenye shule za msingi na sekondari kupitia klabu zilizoanzishwa.

Alisema walimu wamefundishwa na kupewa notisi kwenye vishikwambi juu ya makuzi ya watoto na elimu sahihi ya VVU.

Mkazi wa Kongwa, Juma Hamis alisema mwingiliano wa kibiashara katika Mji wa Kibaigwa unaosababishwa na Soko la Kimataifa la Kibaigwa na maegesho ya malori ya mizigo ndio unaochangia kuwepo kwa maambukizi mapya maeneo hayo.

Chanzo: mwanachidigital