Kutokana na jitihada ndogo za kukabiliana na maambukizi yake, takwimu zinaonyesha watu 71 hupoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Takwimu hizo zilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, yaliyofanyika kitaifa Bariadi mkoani Simiyu ambako alisema ugonjwa huo unaua watu wengi nchini.
Kwa mwaka 2022 alisema maambukizi ya ugonjwa huo yalifika wastani wa wagonjwa 208 katika kila watu 100,000 hukua 25,800 wakifariki.
Asilimia 36 ya waathirika wa Virusi vya Ukimwi wanaopoteza maisha inasababishwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu. Hii inathibitisha ugonjwa huu ni hatari na kikwazo cha maendeleo ya nchi,” alisema Majaliwa. Mwaka 2021 wagonjwa 87,415 waligundulika na kuwekwa kwenye matibabu, lakini watu 44,585 sawa na asilimia 35 hawakubainika, hivyo kuendelea kuwaambukiza wengine. Sambamba na hilo, Waziri Mkuu alizindua mpango mkakati wa kisekta wa kutokomeza Kifua Kikuu ambapo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema unawapata zaidi watu wa kipato cha chini. “Bado kuna jukumu kubwa la kuwatambua wagonjwa wa Kifua Kikuu ili waanze matibabu, ugonjwa huu unatibika endapo mtu atawahi kituo cha afya kwa wakati na dawa zake zipo,” alisema Waziri Ummy. Katika kupambana na ugonjwa huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Tanzania, Dk Florence Temu alisema wamewafikia zaidi ya wahudumu 2,500 wa ngazi ya jamii pamoja na waganga wa tiba asili 1,000 kupambana na ugonjwa huo. “Mgonjwa mmoja anaweza kuambukiza watu 20, hivyo kuibua wagonjwa wengi pamoja na kuwasimamia matibabu ili waweze kupona,” alisema Dk Florence. Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) Tanzania, George Mgomela alisema kwa sasa changamoto kubwa ni usugu wa dawa za Kifua Kikuu. Wakati ikiwa hivyo nchini, kwa Zanzibar pekee, takwimu zinaonyesha wastani wa watu 30 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Fatma Kabole alisema wagonjwa 1,077 wamegundulika kuambukizwa maradhi hayo mwaka 2022, wakipungua kutoka 1,090 wa mwaka 2021.
Wastani wa watu 30 hufariki dunia kutokana na ugonjwa huu hapa Zanzibar kila mwaka na wagonjwa 15 walibainika kuwa na Kifua Kikuu sugu na kuanzishiwa matibabu ya daraja la pili mwaka 2022,” alisema Dk Fatma. Burhana Khamis, mkazi wa Unguja alisema Serikali inapaswa kuongeza nguvu kuwabaini watu wengi walioambukizwa. “Ukiangalia malengo waliyojiwekea kuwabaini wagonjwa 1,600 lakini wamebainika 1,090 hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema
Mpango wa kisekta Mpango wa kupambana na Kifua Kikuu umeandaliwa kuweka hatua zitakazoishirikisha jamii, wafanyabiashara, Serikali na mashirika ya kiraia, ukilenga kutengeneza mbinu za kuwafikia watu walio katika mazingira magumu na kuwapa huduma. Ofisa wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) anayeshughulikia Ukimwi, Kifua Kikuu na homa ya ini, Dk Johnson Lyimo alisema huwa wanaishauri Serikali ili mapambano yawe na mafanikio ni lazima yakabiliwe kisekta. “Tunasema mapambano ya Kifua Kikuu tunataka kuyafanya kisekta kwa sababu ukiangalia vifo vinavyosababishwa nao utaona unawashambulia zaidi watu masikini na wenye matatizo ya lishe,” alisema Lyimo. Alisema mpango huu uliidhinishwa mwaka 2017 katika mkutano wa mawaziri wa afya ulioitishwa na WHO baada ya kudhihirika kuwa katika mapambano ya Kifua Kikuu unahitajika mkakati wa kisekta. Alisema mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2018 uliazimia kila nchi izindue mpango huo. Mwenyekiti wa Muunganiko wa Wadau wa Kutokomeza Kifua Kikuu Tanzania, Dk Peter Bujari alisema ili kuutokomeza wadau wanatakiwa kushirikiana. Dk Bujari alisema malengo ya nchi ni kuhakikisha TB inatokomezwa ifikapo mwaka 2030. “Sisi ndiyo waratibu wa mpango, kazi yetu ni kufuatilia vilivyoahidiwa kama vimefanyika na kuwapa uwezo wa kufanya. Wao wajibu wao ni kufanya, kwa hiyo tutafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha tunawajengea uwezo wa kitaalamu pamoja na kutafuta rasilimali fedha ili kuziwezesha wizara kutekeleza wajibu wao katika kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu,” alisema Dk Lyimo.