Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wenye uzito mkubwa sasa kutibiwa Muhimbili

Watoto Mtoto Child Unene Obesity Watoto wenye uzito mkubwa sasa kutibiwa Muhimbili

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazazi wa watoto wenye uzito mkubwa wameanza mchakato wa kupata Rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya watoto wao.

Mama wa watoto hao, Vumilia Elisha amefika leo Jumatatu, Januari 22, 2024 kwenye ofisi ya Mtendaji Kata ya Makole kwa ajili ya kupata barua ya utambulisho kusudi aipeleke kituo cha afya Makole.

Mchakato huo ni maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo, ili watoto hao waweze kupata matibabu kwa njia ya rufaa.

Profesa Rugajjo amesema njia hiyo ni nafuu tofauti na wao kwenda moja kwa moja hospitalini hapo bila rufaa.

Amesema utaratibu wanaoufuata ni mzuri kwa sababu bila kufanya hivyo, gharama za matibabu zitakuwa kubwa kuliko kufuata rufaa.

Vumilia amesema ameanza kufuatilia rufaa ya matibabu ya watoto wake Imani na Gloria ili waweze kupata matibabu sahihi ya kupunguza uzito walio nao ambao ni mkubwa ukilinganisha na umri wao.

Amelishukuru gazeti la Mwananchi kwa kutoa taarifa za watoto wake na kuleta mwanga wa matumaini wa kupata matibabu ya kupungua uzito kwani walikuwa hawajui cha kufanya.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makole iliyopo Jijini Dodoma, Suzan Yohana amethibitisha kutoa barua ya utambulisho kwa watoto hao ili waweze kupata huduma za matibabu kutokana na tatizo la uzito mkubwa linalowakabili.

“Ni kweli amefika hapa kuchukua barua ya utambulisho ya kuonyesha kuwa ni mkazi wa hapa lakini pia tumeeleza kuwa anahitaji msaada kwa kuwa hana uwezo wa kugharamia matibabu ya watoto wake kutokana na kipato chake kuwa kidogo,” amesema Suzan.

Watoto Imani Joseph mwenye umri wa miaka sita na mdogo wake Gloria Joseph (4) wanakabiliwa na ongezeko la uzito kupita kiasi hali inayowasababisha kushindwa kutembea umbali mrefu pamoja na kuchanganyika kwenye michezo na watoto wenzao.

Imani mwenye zaidi ya kilo 70 na Gloria mwenye zaidi ya kilo 50, wanahitaji matibabu ya kupunguza uzito walionao ili waweze kuwa kama watoto wengine wenye umri wao.

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni uwezo wa wazazi wao wa kugharamia matibabu hayo.

Awali, baba wa watoto hao, Joseph Kalenga aliiomba Serikali na wasamaria wema kusaidia matibabu ya watoto wao kwa sababu hawana uwezo wa kugharamikia matibabu kutokana na kipato cha familia yake kuwa kidogo.

Kalenga amesema Imani kwa sasa ameandikishwa darasa la kwanza, lakini wakati mwingine anashindwa kwenda shuleni kwa sababu anashindwa kutembea umbali mrefu wa kwenda shule na kurejea nyumbani.

“Hata huyu mdogo wake Gloria nimemwandikisha kuanza darasa la awali, lakini mpaka leo hajaanza shule iko mbali na mimi sina hela za kumkodia usafiri. Hivyo naendelea kuwaomba Watanzania wenzangu wanisaidie watoto wangu wapate matibabu,” amesema Kalenga.

Watoto hao ambao wanakula chakula kingi kupita kawaida kwa maelezo ya wazazi wao, wanaweza kumaliza kilo tano za wali na kilo tano za ugali kwa siku moja. Hali hiyo inawafanya wazidi kuongezeka uzito kwa kasi kubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live