Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Watoto wenye ulemavu wasigeuzwe chanzo cha kipato’

D5e0d0a2cdd9440bad81d3758037068b ‘Watoto wenye ulemavu wasigeuzwe chanzo cha kipato’

Wed, 7 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JAMII na vyombo vinavyohusika na ulinzi wa watoto vimetakiwa kutokomeza utumikishwaji wa watoto wakiwamo wenye ulemavu unaofanywa na baadhi ya wazazi kuwafanya kama chanzo chao cha kujipatia mapato.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya The Norbert and Friend Mission ya jijini Arusha, Dk Norbert Mbwiliza, wakati akikabidhi msaada wa viti 15 kwa watoto wenye ulemavu katika kituo cha kutoa huduma kwa watoto wenye ulemavu na vijana cha YDCP kilichopo Tanga.

Alisema si jambo jema watoto hao kutumika kwa ajili ya kuombaomba mitaani kwa ajili ya kulisha familia na kuwanyima haki ya kupata elimu na malezi bora kama watoto wengine.

"Niombe vyombo vinavyoshughulika na ulinzi wa watoto tushirikiane kutokemeza uhalifu unaofaywa na baadhi ya watu kwa kuwatumikisha watoto hao kwani jambo hilo si zuri kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa hili," alisema Dk Mbwiliza.

Mchungaji wa Kanisa la FPCT Tanga, Ayub Mwalumbili alisema watumishi wa Mungu wanaamini kuwa watoto wenye ulemavu ni baraka kutoka kwa Mungu, hivyo wazazi wana jukumu la kuhakikisha wanawalinda watoto hao dhidi ya maovu yote.

Aliwataka wazazi hususani wa kiume kutokimbia familia zao pindi anapozaliwa mtoto mwenye ulemavu, badala yake washirikiane na wenza wao kutimiza wajibu wao wa kulea watoto hao kwa kuwapa haki zao stahiki kama inavyofanyika kwa watoto wengine wasio na ulemavu.

Mwakilishi wa kituo cha YDCP, Joel Mulenga, alisema msaada huo wa viti vya kisasa utakidhi mahitaji ya watoto hao na hivyo kurahisisha shughuli za malezi yao.

"Licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo watoto hawa kwa sasa, hivi viti vitakuwa sehemu ya msaada mkubwa kwao na walezi wao," alisema Mulenga.

Baadhi ya wazazi waliiomba serikali kuona umuhimu wa kukisaidia kituo hicho vifaa vya kisasa kwa ajili ya mazoezi ya watoto wao, badala ya kuendelea kutegemea wahisani pekee.

Mmoja wa wazazi hao, Rashid Karata, alisema kituo hicho kimekuwa sehemu ya msaada mkubwa kwa watoto hao kwani wamekuwa wakipatia mazoezi na malezi yanayowawezesha wengi kumudu kujifanyia huduma ndogondogo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz