Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto pacha wafariki dunia Hospitali ya Bugando

9704 Watoo+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Watoto pacha walioungana tumboni na kifuani waliokuwa wamelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini Mwanza wamefariki dunia kwa matatizo ya upumuaji.

Akizungumza na Mwananchi jana, mkurugenzi mkuu wa BMC, Dk Abel Makubi alisema pacha hao walifariki dunia jana saa 11 alfajiri.

“Hali yao ilibadilika kuanzia saa 9 alasiri ya Julai 31 kwa mfumo wao wa upumuaji kushindwa kufanya kazi, hivyo kuwekwa kwenye mashine maalumu kuwasaidia kupumua hadi mauti yalipowafika wakiwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari, wataalamu na wauguzi waliokuwa wakijitahidi kuokoa maisha yao,” alisema Dk Makubi.

Pacha hao wa kiume walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure Julai 25 na Angela Ramadhan, mkazi wa Nyakato jijini Mwanza.

Saa tatu baada ya kuzaliwa, pacha hao walihamishiwa Bugando kwa ajili ya uangalizi zaidi.

Ofisa uhusiano wa Bugando, Lucy Mogele alisema kifo cha pacha hao kimeusononesha uongozi wa BMC na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla.

Uchunguzi wa timu ya wataalamu na vipimo, ulibaini pacha hao walikuwa wanatumia baadhi ya viungo pamoja ukiwamo moyo, ini na mshipa unaorudisha damu kwenye moyo.

Hata hivyo, kila mmoja alikuwa anajitegemea kwa kuwa tumbo lake, mapafu na figo.

Chanzo: mwananchi.co.tz