Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto milioni 8 wafikiwa na huduma jumuishi za afya

A120e704be1af798f64ec078c1c4ba08 Watoto milioni 8 wafikiwa na huduma jumuishi za afya

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya watoto milioni nane wenye umri kuanzia miezi sita hadi miaka mitano Desemba mwaka jana wamefikiwa na huduma jumuishi za afya na lishe ambazo hutolewa kila baada ya miezi sita.

Mkurugenzi Idara ya Sayansi Chakula na Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini, Eliphatio Towo alisema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari kuhusu Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto jijini Dar es Salaam.

Towo alisema huduma hiyo inatolewa kwa kuwa moja ya matatizo makubwa ya lishe hapa nchini ni upungufu wa Vitamin A.

“Kwa mujibu wa utafiti wa Afya na Demografia wa mwaka 2010 takribani asilimia 33 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano walibainika kuwa na upungufu wa vitamin A mwilini. Upungufu wa vitamin A mwilini husababisha madhara mengi kwa mtoto, ambayo miongoni mwa hayo ni pamoja na ukosefu wa kinga mwilini na hivyo mtoto kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mara kwa mara, kutoona vizuri katika mwanga hafifu na mengine mengi,” alisema.

Alisema mwezi huo wa afya na lishe ya mtoto ni mojawapo ya mikakati ya kulinda afya na maendeleo ya mtoto ambapo katika kipindi hiki huduma jumuishi za afya na lishe hutolewa kwa watoto wenye umri huo.

Alitaja huduma zinazotolewa ni utoaji wa matone ya vitamin A, utoaji wa dawa za kutibu maambukizi ya minyoo, upimaji wa hali ya lishe, utoaji ushauri nasaha na kutoa rufaa kwa mtoto anayebainika kuwa na utapiamlo mkali.

Towo alisema huduma hizo zimekuwa zikitolewa kila baada ya miezi sita ambayo ni Juni na Desemba kila mwaka na kuwafikia watoto wengi zaidi na kuongeza kuwa pamoja na huduma hizo zinazotolewa katika miezi hiyo kumekuwa na uhamasishaji kuhusu ulaji vyakula vyenye vitamin A kwa wingi.

Chanzo: habarileo.co.tz