Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto milioni 10 kupatiwa chanjo ya polio nchini

76f9d95e729ab38a36495b108a4afaf4 Moja ya watoto akipatiwa chanjo ya Polio

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watoto zaidi ya milioni 10 wenye umri wa chini ya miaka mitano watapatiwa chanjo ya matone ya polio kuanzia kesho nchi nzima.

Ofisa Programu kutoka Wizara ya Afya katika Mpango wa Taifa wa Chanjo, Lotalia Gadau alisema hayo jijini Dodoma kwenye semina ya wahariri wa vyombo vya habari.

Alisema kampeni hiyo itafanyika kwa awamu nne na kwamba awamu ya kwanza imefanyika katika mikoa minne inayopakana na nchi ya Malawi ya Njombe, Mbeya, Ruvuma na Songwe.

Alisema awamu ya pili itafanyika kwa siku nne kuanzia kesho hadi Mei Mosi, mwaka huu na itakuwa ya nyumba kwa nyumba na itazinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Gadau alisema kuna dozi za chanjo hiyo zaidi ya milioni 13.32 na kwamba

hutolewa kwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano bila kujali hali zao za chanjo za awali.

"Hivyo wazazi na walezi wanapaswa kujitokeza kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hii hata kama amepata chanjo jana, tunampatia hii na pia akishapata hii chanjo na siku anayofuata anaratiba ya kwenda kliniki kumpa chanjo basi mpeleke, chanjo hizo hazina madhara yoyote," alisema Gadau.

Alisema mara ya mwisho kupata mgonjwa wa polio nchini ilikuwa mwaka 1996 mkoani Mtwara na mwaka 2015 Tanzania ilipata cheti kutoka Shirika la Afya Duniani cha kuonesha hakuna ugonjwa huo nchini.

Alitoa mwito kwa vyombo vya habari kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.

"Kwa awamu ya kwanza tumevuka lengo tuliloweka, tulipata idadi kubwa. Kutakuwepo na timu za uchanjaji na uhamasishaji itapita nyumba kwa nyumba na chanjo hii haina kitu nyuma yake bali inalenga kumfikia kila mtoto popote alipo hata kwenye nyumba za ibada," alisema.

Mratibu wa Kampeni ya Kutokomeza Ugonjwa wa Polio Tanzania, Dk Anthony Kazoka alisema polio ni ugonjwa unaotakiwa kutokomezwa duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live