Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto 70 wabainika kuwa na usonji

0ad8bd69e4162aa96c387d1d3c4d3391 Watoto 70 wabainika kuwa na usonji

Fri, 13 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya watoto 70 mkoani Mwanza wamebainika kuwa na tatizo la usonji na sababu za tatizo hilo bado hazijafahamika.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Living Together Autistic Foundation (Li-TAFO), Shangwe Mgaya, alibainisha hayo alipozungumza na HabariLEO juu ya maandalizi ya mkutano wa siku moja, utakaofanyika Novemba 15 mwaka huu jijini hapa.

Mkutano huo utahudhuriwa na washiriki 150 kutoka taasisi mbalimbali na familia za watoto wenye usonji. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella atakuwa mgeni rasmi.

"Kwa sasa watoto hao kwa kushirikiana na madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando tunawafanyia unasihi ikiwemo kuwaeleza wazazi wao washiriki kwenye mazoezi ya viungo na kuongea nao kwa sababu hadi sasa tiba ya usonji bado haijapatikana," alisema.

Alisema kati ya watoto hao waliobainika kuwa na usonji, 10 wanapatiwa mazoezi ya viungo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando. Wengine wazazi wao wameshauriwa kuwapeleka Kilimanjaro, ambako wanaweza kupata huduma ya mazoezi ya viungo.

"Kwa sasa hakuna shule au hospitali inayowasaidia watoto wenye usonji hadi wapelekwe mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam ambako wanaweza kupatiwa huduma," alisema.

Mgaya ambaye pia ni mama mwenye mtoto mwenye usonji, Daniel Mgao (9) alisema alianzisha Taasisi ya Li-TAFO kutokana na kunyanyapaliwa na familia ya mumewe kwa sababu ya kuzaa mtoto mwenye usonji. Alisema unyanyapaa huo ulisababisha ndoa yao kuvunjika

"Nilianzisha taasisi hii ili kuwasaidia watoto wenye usonji, lakini pia kujenga uelewa kwa jamii kuhusu usonji na kuweka mikakati chanya ya namna ya kukabiliana nao," alisema,

Aliongeza: "Tatizo la usonji hapa nchini ni kubwa, Hospitali ya Rufaa ya Bugando hapa Mwanza hupokea watoto wawili hadi watatu kwa wiki wenye matatizo ya usonji".

Usonji ni changamoto iliyopo kwenye mfumo wa ufahamu inayomsababisha mtoto kushindwa kuwasiliana, kuchangamana na wengine na kushindwa kuzoea mazingira mapya, hivyo kuharibu hisia na tabia zake.

Alisema lengo la mkutano huo ni kujenga uelewa kwa washiriki na familia zenye watoto wenye usonji na kuzitia faraja.

“Katika mkutano huo, watu mbalimbali watapata fursa ya kuwachangia watoto wenye usonji na familia zao ili waweze kutumia fedha zinazopatikana kufanyia mazoezi na mahitaji mengine muhimu,” alisema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Li-TAFO inatarajia kujenga kituo kikubwa jijini Mwanza ili kuwawezesha watoto wenye usonji, kujifunza mambo na ujuzi mbalimbali kadiri ya vipaji vyao.

“Kituo hicho kitakuwa na madarasa ya kujifunzia, ofisi, hosteli na kumbi za mikutano, ambapo zaidi ya shilingi milioni 500 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz