Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto 3,000 wakabidhiwa kadi za bima ya afya

Csm NHIF D1731a8d98 Watoto 3,000 wakabidhiwa kadi za bima ya afya

Wed, 4 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la World Vision Tanzania limekabidhi kadi za bima ya afya (CHF) iliyoboreshwa kwa watoto 3,000, kadi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) za watoto 10 na shuka jozi 3,278 kwa watoto wanaishi katika mazingira hatarishi wilayani Kilosa , mkoani Morogoro, vyote hivyo vikiwa na thamani ya Sh milioni 52.8.

Meneja Mradi wa shirika kwa upande wa Tarafa ya Magole na Ulanga wilayani humo, Elisei Chilala alisema hayo hivi karibuni kuwa shirika hilo limetoa madawati 160 yenye thamani ya Sh 13,216,000 na kadi za bima ya afya za CHF kwa watoto 3,000 zenye thamani ya Sh 15,000,000.

Chilala alisema vitu hivyo vimefadhiliwa na shirika hilo ambalo linafanya kazi katika Tarafa za Magole na Ulaya wilayani Kilosa kupitia miradi mbalimbali katika sekta ya afya, lishe, maji, elimu na utetezi.

Alisema shirika hilo pia limetoa kadi za NHIF kwa watoto 10 wenye mahitaji maalumu zenye thamani ya Sh 504,000 na mashuka vipande 3,278 kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi vikiwa na thamani ya Sh 24,585,000.

Meneja huyo alikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Loata ole Sanare kwa niaba ya uongozi wa shirika hilo.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro licha ya kushukuru kwa ajili ya vifaa hivyo, alisema serikali inatambua misaada mbalimbali inayotolewa na World Vision .

Pamoja na hayo aliliomba shirika hilo kuendelea kufanya kazi na halmashauri na kulitaka kuongeza wigo wa kufanya kazi kwa mapana zaidi katika tarafa nyingine wilayani Kilosa na mkoa wa Morogoro.

Mkuu wa mkoa alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi ya Kilosa na mkoa wa kiujumla kujitokeza kukata kadi za bima ya afya kwa ajili ya familia zao, kwani kadi hizo ni muhimu na zinasaidia kupata matibabu kwa urahisi hata nyakati ambazo mtu anakuwa hana fedha kwa ajili ya matibabu.

Kuhusu msaada wa madawati, alisema mkoa huo umeweka mkakati wa kuwa na shule ya bweni hususani kwa shule za sekondari ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vishawishi vinavyosababishia kupata mimba na kukatisha ndoto zao na kutaka kuwepo kwa ushirikiano baina ya serikali na wazazi ili kufanikisha jambo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi alisema shirika hilo limekuwa mdau namba moja katika kutoa misaada mbalimbali ili kupambana na umaskini .

Chanzo: habarileo.co.tz