Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto 20 kuzibuliwa mishipa na kuzibwa matundu ya moyo kwa Cath Lab

Tue, 28 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi  ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child's Heart-SACH) ya nchini Israel kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wanatarajia kutoa matibabu ya upasuaji wa njia ya tundu dogo kwa watoto 20 wenye matatizo ya matundu na hitilafu ya mishipa ya damu katika moyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Mei 27, 2019 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi wakati akitambulisha wajumbe wa bodi ya SACH ambao kwa miaka sita mfululizo wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto.

Amesema zaidi ya watoto 400 wamenufaika kwa kufanyiwa upasuaji kupitia fedha hizo, hivyo bodi imeona ni vema kufika kwa ajili ya kuona kazi hiyo inavyofanyika.

“Hii ni mara yao ya sita wanakuja kufanya upasuaji wa watoto na safari hii imekuwa ni tofauti kidogo wamekuja na wajumbe wa bodi kwa ajili ya kuja kuangalia utekelezaji wameongozana na madaktari bingwa pia kutoka Israel, kwa ajili ya kufanya upasuaji kwa watoto 20,” amesema.

Profesa Janabi amesema Israel wamekuwa wakiisaidia Tanzania kwa muda mrefu kwa kusomesha madaktari bingwa wa tiba za moyo kwa watoto na kwamba, Canada imekuwa ikitoa fedha nyingi kuwekeza katika mafunzo ya mabingwa hao na hata matibabu kwa watoto.

“Tunatarajia watoto 20 watafanyiwa upasuaji mpaka kufikia Ijumaa tutakamilisha. Januari mwaka huu, walikuja wakafanya upasuaji na daktari wetu bingwa Mtanzania mmoja akawa anaendelea kufanya upasuaji huu kutumia tundu dogo na sasa wamekuja ili kutuongezea ujuzi zaidi, kwa sababu ina faida kubwa,” amesema na kuongeza;

Pia Soma

“Kwanza muda mchache unatumika kuwatibu watoto na wanakwenda nyumbani na inaokoa gharama pia ya matibabu.”

Mkurugenzi Mtendaji wa SACH, Simon Fisher amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto wengi wenye uhitaji, “zaidi ya watoto 400 wamenufaika na Save the Child's Hearts.”

Chanzo: mwananchi.co.tz