Serikali imepitisha na kusambaza mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya msaada wa akili na kisaikolojia utakaowabana watoa huduma wasio na weledi wa kutosha.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwajuma Magwiza wakati akifungua kikao cha kupitisha na kusambaza mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya msaada wa akili na kisaikolojia.
Alisema pamoja na jitihada zinazaofanywa na serikali huduma hizo zimekuwa zikitolewa na watoa huduma wasio na weledi wa kutosha bila uratibu na kusababisha jamii kukosa huduma hiyo muhimu na kuendelea kuathirika.
Alisema mwongozo huo wa kitaifa na taratibu hizo zimeandaliwa kwa lengo la kuwaelekeza na kuwawezesha watoa huduma kutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa utaratibu , ubora na uendelevu katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa ujumla.
Alisema kuwa serikali inatambua kuwa utekelezaji wa taratibu hizi unahitaji ushirikiano na kuhusisha watendaji na wadau mbalimbali katika kushughulikia mahitaji ya kisaikolojia na kijamii.
Alilishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) kwa kudhamini, kupitisha na kusambaza mwongozo huo na kuwezesha waalikwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara kufika kwenye kikao hicho.
Magwiza alisema Tanzania inakabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazotokana na umaskini, kudhoofika kwa mifumo ya jadi ya hifadhi ya jamii, maafa, ukosefu wa ajira, magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama saratani, kisukari na shinikizo la damu.
Aidha, alisema changamoto hizi zimeathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa kisaikolojia na kijamii kwa mtu mmoja mmoja, familia, kaya na jamii kwa ujumla.
Alibainisha kuwa maendeleo makubwa yamefanyika nchini kutokana na sera na misingi ya kisheria ili kukabiliana na changamoto hizo.
Alisema kuwa Sera na misingi hiyo ya kisheria ni pamoja na Sera ya Taifa ya Afya ya 2007, Sera ya Taifa ya Wazee ya 2003, Sera ya Taifa ya Watu wenye ulemavu ya 2004 na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya 2008,.
Pia Sheria ya Kuzuia Usafirishaji wa Binadamu ya 2008, Sheria ya Mtoto ya 2009, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya 2010, na Mpango wa kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017-2022"alisema