Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoa huduma wanaopuuza kadi bima ya afya waonywa

Bimapiic Data Watoa huduma wanaopuuza kadi bima ya afya waonywa

Tue, 9 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewaonya watoa huduma za afya wanaopuuzia bima za afya kuacha tabia hiyo, kwani wanarudisha nyuma mchakato wa bima ya afya kwa wote.

Shigella ametoa kalipio hilo wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kasamwa, Kata ya Kasamwa Halmashauri ya mji wa Geita.

Amesema, ofisi yake imebaini baadhi ya wauguzi na madaktari wanatoa kipaumbele zaidi kuwahudumia watu wanaolipa pesa taslimu kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuwakacha wenye bima.

Ameeleza, hali hiyo imesababisha wananchi wengi kupata kigugumizi kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa kwa kuwa hawathaminiwi wanapohitaji huduma tofauti na wenye fedha taslimu.

“Kwa hiyo rekebisheni ili watu wajiunge kwenye bima ya afya, ili wapate matibabu ya uhakika, matibabu ya uhakika yanasaidia sana wananchi.

“Wakati mwingine tunashindwa kupata matibabu kwa sababu wakati tunaugua tunakuwa hatuna fedha, na sisi tunafahamu, ugonjwa hauna tarehe, hauna saa na wala hauna muda.

“Kwa hiyo njia pekee ya kujiimarisha na kupata huduma ya uhakika ni kujiunga na bima ya afya, ili tuwe na uhakika wa kupata huduma za bima ya afya,” amesisitiza.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inafanya juhudi kubwa kuboresha huduma za afya, ikiwemo dawa na vifaa tiba ambapo alielekeza vituo vya afya kuzingatia utoaji wa huduma stahiki.

“Katika mkoa wetu dawa zimeongezeka zaidi ya mara tatu, lakini nina uhakika wapo watu wanaenda kutibiwa hata ‘panadol’ hawapati.

“Nimemuelekeza DMO mfuatilie na mrekebishe mapungufu, najua madaktari na wauguzi wanatoa huduma nzuri, lakini wapo baadhi wanapenda kuficha dawa bila utaratibu.

“Sasa kabla hatujaanza kuwawekea vyombo vya kuwafuatilia rekebisheni haya mapungufu, ili mgonjwa akienda kutibiwa aweze kupata zile dawa,” ameelekeza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live