Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WaterAid yakabidhi vituo 12 vya kunawa mikono Dar

ETFjJB4XQAErEbO WaterAid yakabidhi vituo 12 vya kunawa mikono Dar

Sat, 16 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia watanzania kunawa mikono ili kupambana na maambukizi ya Uviko 19, Shirika lisilo la Kiserikali la WaterAid limekabidhi vituo 12 vya kunawa mikono vyenye thamani ya Sh144 milioni katika mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Ijumaa Oktoba 15, 2021 katika makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika hilo, Anna Mzinga amesema maeneo yaliyonufaika na vituo hivyo ni Hospitali ya Mwananyamala, Mnazi Mmoja, Temeke, Kituo cha Magufuli, Shule ya Msingi Malamba Mawili na Msasani, Stendi ya mabasi mawasiliano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Amesema msaada umetolewa na shirika hilo kwa kushirikiana na Shirika la The Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO) na Unilever ambapo msaada huo unalenga kuendeleza mapambano ya ugonjwa wa Uviko 19.

"Tunatambua bila huduma sahihi ya maji, usafi wa mazingira na vifaa vya kunawia mikono kwenye makazi yetu, shuleni, vituo vya kutolea huduma za afya basi mazingira yetu yatakuwa ni vyanzo vya magonjwa na kuacha jamii ikiwa katika hatari ya kupata milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na kuingia kwenye gharama kubwa za matibabu, " amesema

Hata hivyo amesema unawaji mikono umesaidia nchi katika mapambano ya ugonjwa wa Uviko-19.

Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume amesema Serikali itaendelea kuwekeza nguvu katika unawaji sahihi wa mikono ili kuendelea kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado eneo hilo la unawaji wa mikono linapewa nafasi ndogo katika baadhi ya maeneo hivyo amehimiza jamii kuendelea kunawa ili kujikinga na magonjwa yanayoambukiza.

Chanzo: mwananchidigital