Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watendaji idara ya maendeleo Dar wapewa somo la corona

Watendaji idara ya maendeleo Dar wapewa somo la corona

Sat, 28 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watendaji zaidi ya 170 wa idara ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania wamepewa elimu juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ili wawafikishie wananchi na wafanyabiashara wadogo wanaopatikana katika mitaa na wilaya zao.

Mafunzo hayo ya siku moja yametolewa kwa watendaji kutoka wilaya ya Ubungo, Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na halmashauri ya jiji.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo leo Jumamosi Machi 28,2020 Katibu Mkuu Wizara ya Afya anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Wazee, Jinsia na Watoto, Dk John Jingu amesema wameamua kuwatumia maofisa hao kufikisha elimu kwa wananchi kwa sababu wao huweza kufika hadi ngazi ya chini Zaidi.

“Tunataka elimu hii iwafikie wengi zaidi kwa sababu kama nchi bado hatujafikia hatua ya kufunga biashara zetu sasa ili tusifikie huko tuwaelekeze wafanyabiashara hawa namna ya kujikinga na maambukizi ya corona,” amesema

“Mama ntilie waelekezeni kufanya biashara zao vizuri, watu wapeane nafasi wanapokwenda kukaa kula na wakikaa wasiangaliane ili mtu akipiga chafya asiweze kumuambukiza mwenzie kwa haraka,” amesema Dk Jingu

Amesema elimu hiyo iwafikie pia wamiliki wa maduka wajifunze namna ya kuwahudumia watu wakiwa wamekaa mbali nao ili wasipate maambukuzi.

Pia Soma

Advertisement

“Wakati baadhi ya nchi shughuli zote zikifungwa ikiwamo maduka kuna baadhi ya watu ili wale ni lazima watoke nje sasa ni bora tuzidi kujikinga ili tusifike hatua ya kumwambia mtu asitoke ndani ili ajikinge na corona halafu apoteze maisha kwa sababu ya njaa,” amesema

Kwa upande wake, Ofisa maendeleo ya jamii kutoka wilaya ya Temeke, Shamira Hassan ambaye ni mmoja kati ya waliopatiwa mafunzo amesema semina hiyo imewaongezea ufahamu zaidi kabla hawajakwenda kuielimisha jamii ili waweze kujikinga na ugonjwa huo.

“Tumelifurahia suala hili kwa sababu tukienda kuwaelimisha mama lishe, wauza maduka tutakuwa na uhakika na kile tunachokizungumza,” amesema Shamira.

Chanzo: mwananchi.co.tz