Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watembea kilomita 10 kufuata huduma ya dharura

335fb9520a42e1cd865388b1d5988021.jpeg Watembea kilomita 10 kufuata huduma ya dharura

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI wa kijiji cha Mlembule Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 10 kutafuta huduma za dharura zikiwemo za upasuaji kutokana na kukosa kituo cha afya.

Akizungumza Mwenyekiti wa kijiji hicho Bahatisha Bahatisha alisema hali hiyo inawaathiri sana wajawazito.

Alisema pamoja na umbali huo wakati wa mvua hali huwa mbaya kutokana na kuwepo kwa korongo la Manamba ambalo hujaa maji na hivyo kuvuruga usafiri. Aidha barabara ni mbovu.

Bahatisha alisema kutokana na hali hiyo wajawazito wamekuwa wakijifungulia njiani au kwa wakunga wa jadi .

Mmoja wa wananchi, Eva Deo alisema katika kipindi cha masika maisha yao yanakuwa hatarini hasa kutokana na kuwa na uwezo finyu wa kufika makao makuu ya wilaya ambako ndiko matibabu yanakopatikana.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Erichard Rwezahura alikiri kuwapo na changamoto hiyo na uhitaji wa kituo cha afya katika kata hiyo .

Hata hivyo alisema katika mwaka wa Fedha wa 2021/2022 halmashauri imetenga kiasi cha Sh milioni 50 kwa ajili ya kumalizia zahanati iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.

Dk Rwezahura alisema pamoja na kumalizia zahanati hiyo pia amewataka wakazi wa kijiji hicho kutafuta huduma katika vijiji vya karibu kama Mwezele na Tambi.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mwezele Rose Maganga alisema wahudumu wa afya wa kijiji hicho huja kuwapima akina mama na watoto katika ofisi ya mtendaji wa kijiji kitu kinacho wakosesha faragha na usiri .

Chanzo: www.habarileo.co.tz