Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Macho Duniani, jamii imetakiwa kujenga utaratibu wa kupima macho mara kwa mara ili kuepuka matatizo ya upofu.
Siku ya Macho Duniani huadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Afya ya Macho kwa wote na huduma za macho popote ulipo'.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 11, 2018, daktari bingwa wa magonjwa ya macho na upasuajiĀ kutoka hospitali ya macho ya Agarwal, Emeritus Chibuga amesema asilimia moja ya watu duniani wana tatizo la uoni hafifu.
"Uoni hafifu unaweza kusababisha mtu kupata upofu na hii inatokana na jamii kutokuwa na utaratibu wa kwenda hospitalini kupima macho mara kwa mara," amesema.
Hata hivyo ametaja wazee kuwa ni kundi la watu ambao wapo katika hatari ya kupata upofu kutokana na lenzi ya macho kukua kila siku.
"Hizi lenzi zinakuwa kila siku kwa hiyo mtu anapofikisha miaka 45 na kuendelea lenzi inakuwa kubwa zaidi na kusababisha upofu hivyo tunawashauri kuhudhuria vituo vya afya ya macho mara kwa mara kupata ushauri," amesema.
Ameomba Serikali kutoa kipaumbele kwenye matatizo ya macho kwani ni sekta ambayo inasahaulika.
Aidha ameomba Serikali kujenga vituo vya afya vya macho kila wilaya ili kuwasogezea wananchi huduma.
Naye mratibu wa afya ya macho mkoani Dar es Salaam, Dk Patrick Kabangutse amewataka wananchi kutumia nafasi hii ya kupima macho bure kwa kujitokeza kwa wingi.
"Kuanzia zoezi la upimaji limeanza Jumapili mpaka leo watu 2600 wamejitokeza kupima hata hivyo idadi hiyo ni ndogo hivyo hii ni nafasi kwao kutambua afya ya macho,"amesema.
Kuhusu wataalamu wa macho Dk Kabangutse amesema kuna uhitaji mkubwa wa madaktari wa macho kwani baadhi ya hospitali za serikali hawapo.
Wakizungumza wakati wa zoezi la upimaji wa macho katika hospitali ya Mwananyamala baadhi ya wananchi wamesema Serikali iandae utaratibu wa kupima watu macho bure bila malipo.
Hamisi Mbuya mkazi wa Mwananyamala A amesema anatamani kupima macho mara kwa mara lakini hana uwezo wa kifedha.
Naye Mwanahamisi Issa amesema huduma ya kupima macho bure isisubiri hadi siku ya maadhimisho bali iwe endelevu.