Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania wahimizwa kupima haemophilia, inaua

Haemopholia Damu.png Watanzania wahimizwa kupima haemophilia, inaua

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imezindua kliniki ya ugonjwa wa Haemophilia huku wakazi wa kanda hiyo wakihimizwa kujitokeza kupima na kupatiwa matibabu.

Haemophilia ni ugonjwa wa kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili kunakosababishwa na damu ya mgonjwa kukosa chembe protini, jambo linaloifanya isingande huku madhara ya ugonjwa huo yakitajwa kuwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu au kifo.

Akizindua kliniki hiyo jana Septemba 27, 2022 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalage amesema mbali na Bugando, hospitali nyingine zitakazotoa matibabu hayo ni pamoja na hosputali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali ya kanda ya Mbeya, Benjamini Mkapa (Dodoma), hospitali ya mkoa wa Morogoro, na KCMC mkoani Kilimanjaro.

“Kliniki hizi tumeziwezesha vifaa tiba, wataalamu, dawa na vifaa vya mazoezi kwa wagonjwa lengo likiwa ni kupanua wigo wa utambuzi wa wagonjwa wa haemophilia mapema ili waanze matibabu,” amesema Dk Shekalage.

Kwa upande wake, mratibu wa haemophilia nchini, Dk Stella Rwezaula amesema wagonjwa 20 kati ya 360 waliotambuliwa nchini wanatoka kanda ya Ziwa huku takwimu zikionyesha mtanzania mmoja kati ya 10,000 ana ugonjwa huo.

“Dalili za ugonjwa huo huonekana utotoni mfano mtoto akikatwa kitovu, jino likiota ama akifanyiwa tohara, mgonjwa atatokwa damu nyingi zisizokata na kupelekea kuhitaji kuongezwa damu.

“Ukiona dalili hizo muwahishe mtoto hospitalini akafanyiwe uchunguzi mapema,” amesema Dk Rwezaula.

Ili kuongeza uelewa na utambuzi wa ugonjwa huo, mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Mseru amesema juhudi zinahitajika kutokomeza ugonjwa huo ambao ni miongoni mwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele nchini.

“Tunataka kuhakikisha watu wenye haemophilia wanatambulika wakati ugonjwa haujafika katika hatua mbaya. Tumeshapata vifaa tiba na vitendanishi vyenye thamani ya Sh181 milioni na mpaka sasa watalaam 381 wamepewa mafunzo kuhusu ugonjwa huu nchi nzima," amesema Profesa Mseru.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live