Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania milioni moja kufanya usafi siku ya Usafi Duniani

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kuelekea siku ya Usafi Duniani, watu milioni 1.1 nchini ambao ni sawa na asilimia 5 ya wenye umri wa kufanya kazi wanatarajiwa kushiriki katika kusafisha maeneo yaliyokithiri kwa uchafu nchini. 

Katika siku hiyo ya Septemba 15 ambapo Tanzania inaungana na nchi 150 duniani kote katika kuazimisha siku ya usafi, jumla ya tani 16,500 za uchafu unaotupwa kinyume cha sheria zitakusanywa. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 9 Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali Nipe Fagio, Tania Hamilton amesema kila mwaka Tanzania inapoteza fedha nyingi kwa kutibu magonjwa ya mlipuko na kukabiliana na athari za mafuriko yanayosababishwa na utupaji taka na uchafuzi wa mazingira.

"Ukitupa taka hovyo mitaro itaziba na kuleta athari. Tunaamini kupitia siku hii na idadi hiyo ya watu tunaweza kuboresha zoezi la usafi, kutengeneza mazingira ya kibiashara, kutangaza utalii na watu kufurahia mazingira salama katika ufanyaji wa shughuli binafsi na kijamii," amesema Tania Hamilton. 

Mjasiriamali Fortunatus Ekklesiah amesema mwaka 2012, Jarida la Forbes liliitaja Tanzania katika nafasi ya 12 kwa uchafu duniani jambo ambalo linatia aibu. 

"Tuna mengi ya kujivunia kama nchi yanayoweza kutupa sifa nzuri tofauti na hiyo, tukiweza kuzuia utupaji hovyo wa taka na vifo vitokanavyo na uchafuzi wa mazingira vitapungua," amesema Ekklesiah. 

Jumla ya vituo 30 katika jiji la Dar vitatumika katika ukusanyaji wa uchafu katika maadhimisho hayo huku mikoa 7 ikiwa na vituo 2 kila mmoja. 

Chanzo: mwananchi.co.tz