Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watano kutibiwa mshipa wa moyo bila upasuaji JKCI

Moyo Dalili Shida Watano kutibiwa mshipa wa moyo bila upasuaji JKCI

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wagonjwa watano wanatarajiwa kufanyiwa matibabu ya kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka bila kupasuliwa kifua na tumbo.

Upasuaji wa aina hiyo utafanyika kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini India na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Matibabu hayo ni mwendelezo wa tiba za kibingwa na ubingwa bobezi zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania.

Tiba hiyo inafanyika kupitia njia ya tundu dogo, ambapo mgonjwa anawekewa kifaa maalumu kwenye mshipa huo kwa muda wa saa mbili na ataendelea vizuri tofauti na akipasuliwa.

Akazungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Upasuaji Taasisi ya JKCI, Dk Angela Muhozya amesema mgonjwa mmoja ameshafanyiwa jana na leo watafanyiwa wagonjwa wengine watatu.

“Tofauti na upasuaji wa kufungua kifua na tumbo tunatumia zaidi ya saa 10 na tunatumia damu nyingi, lakini hii hapa tunatumia saa mbili pekee, hivyo matibabu haya yatapunguza kwa kiasi kikubwa muda na madhara kwa mgonjwa,” amesema Dk Muhozya.

Amesema kupitia matibabu hayo, wataalamu wa JKCI wanapata ujuzi kwa kuwa wanaupata kutoka kwa madaktari hao kutoka India kwenye kambi hiyo ya wiki moja.

Kwa upande wake, daktari bingwa upasuaji wa moyo, kifua na mishipa ya damu JKCI, Dk Alex Joseph amesema kifaa hicho kinawekwa katikati ya mshipa uliotanuka, ili kuzuia usichanike.

“Aina hii ya matibabu inapunguza hatari ya kifo kwa asilimia tano hadi sita, ni tofauti na ile ya upasuaji wa kuchana tumbo na kifua ambayo hatari ya kifo ni asilimia 45,” amebainisha Dk Joseph.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema wameshirikiana na wataalamu takriban watano kutoka India ambapo kwa mgonjwa mmoja inagharimu Sh80 milioni.

“Wangeenda India mgonjwa mmoja ingegharimu Sh150 milioni, hivyo kimeokolewa kiasi kikubwa cha fedha. Tunashukuru Serikali imetoa Sh900 milioni, ili kuwafanyia upasuaji wagonjwa hawa,” amesema Dk Kisenge.

Akizungumzia sababu ya matatizo ya mishipa ya damu kutanuka na kupasuka ghafla, amesema hasa inatokea kwa wale wanaovuta sigara, unene, unywaji wa pombe uliokithiri, kutotibiwa vizuri kwa wagonjwa wa shinikizo la juu la damu.

Amesema tatizo hilo lipo na kuna wagonjwa zaidi ya 30 wanasubiri matibabu hayo na kwamba hao ni kabla ya kwenda mikoani.

Naye, daktari mbobezi katika timu hiyo iliyotoka India, Dk Gireesh Warawdekar amesema moja ya faida watakayoipata Tanzania ni kupata ujuzi huo mkubwa na wa kisasa wa matibabu ya mishipa ya moyo ambayo inapita hadi tumboni.

“Tumekuja kwa ushirikiano na JKCI kufanya matibabu haya na tutakuja tena kuweka kambi, ambapo hapo baadaye watalaamu wa hapa wataweza kufanya wenyewe,” amesema Dk Warawdekar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live