Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kuongeza uzalishaji dawa

167955befa2163595fb809d64651d56b Watakiwa kuongeza uzalishaji dawa

Wed, 21 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZALISHAJI wa dawa na vifaa tiba wametakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji dawa kwa kushirikian na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Afya), Profesa Abel Makubi alitoa mwito huo jana Dar es Salaam alipotembelea Bohari Kuu ya Dawa na kuzungumza na wazalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

"Tunawashukuru kwa uzalendo wenu wa kuwekeza nchini, pokeeni salamu kutoka kwa Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima na manaibu waziri," alisema.

Hata hivyo, Profesa Makubi aliwataka wazalishaji hao kushirikiana na MSD kuhakisha dawa zao zinawafikia wananchi wa vijijini ili kutatua changamoto ya uhaba wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Aliwahakikishia wazalishaji hao kuwa serikali ipo tayari kushirikiana nao na kuhakikisha eneo la uzalishaji dawa linakua ili kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi.

"MSD ni chombo chetu cha kuwatumikia wananchi, hivyo ni vyema kukipa ushirikiano ili upatikanaji wa dawa, vifaa na vitendanishi uwapo wakati wote," alisema.

Kwa upande wa bei za bidhaa za dawa, Profesa Makubi aliwataka wazalishaji kukaa pamoja na MSD kupitia upya bei ili ziwe na uhalisia wa soko bila kuumiza wananchi.

Aliahidi kuwa serikali itawalipa kwa wakati wazalishaji wote ambao watatoa ushirikiano wa kutoa dawa na vifaa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Wazalishaji hao ambao ni wamiliki wa viwanda vya dawa na bidhaa nyinginezo za afya nchini, wameahidi kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuboresha upatikanaji wa dawa nchini na kuuunga mkono serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Chanzo: www.habarileo.co.tz