Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya leo

3f657fa3349d15a43f17b9a1612c8528 Watakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya leo

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI wa jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi leo katika viwanja vya Mnazimmoja kwa ajili ya kupima afya zao bure pamoja na kupata elimu ya afya juu ya magonjwa mbalimbali hususan yasiyoambukiza.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alitoa wito huo jana alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu Maadhimisho ya Magonjwa Yasiyoambukiza ambayo kilele chake ni Novemba 14, mwaka huu.

Alisema kuanzia leo hadi Novemba 14 katika viwanja hivyo kutatolewa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo.

“Kila mmoja ajitahidi kutumia siku hizo vizuri kwa ajili ya kupima na kufanyiwa uchunguzi wa afya kwani huduma hizo itakuwa ni bure,” alisema.

Dk Mfaume alisema pamoja na huduma hizo za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, pia kutakuwa na uchunguzi wa magonjwa jumuishi ya yanayoambukiza.

"Magonjwa ambayo yatachunguzwa ni yale yasiyoambukiza, makundi makubwa ya magonjwa hayo ni kisukari, magonjwa mbalimbali ya saratani, kuna aina nyingi sana za saratani mnazifahamu, lakini pia kuna magonjwa ya moyo na kiharusi, hayo ni baadhi tu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza yatapewa kipaumbele.”

"Lakini kuna magonjwa ya kudumu ya mfumo wa upumuaji, mfumo wa njia ya hewa, lakini kuna makundi mengine kwa mfano magonjwa ya afya ya akili nayo pia yataangaliwa, tuna magonjwa ya selimundu, tuna magonjwa ya macho, huduma za macho zitakuwa zinatolewa hapa na kuchunguzwa pia kwa hiyo ni huduma mbalimbali zitatolewa," alisema.

Alisema kutakuwapo wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambao watachunguza saratani mbalimbali ikiwa ni sehemu ya magonjwa yasiyoambukiza wakiwemo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Alisema pia wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Damu Salama watakuwepo na wadau mbalimbali kutoka hospitali za Aghakhan na TMJ.

Aliwataka wananchi wasisubiri siku ya mwisho ndio wajitokeze bali wafike leo kwa wingi kwa kuwa wataalam wamejiandaa kwa vifaa na huduma zitatolewa bila malipo isipokuwa watakaohitaji rufaa ambapo mgonjwa akienda kwenye vituo vya afya atachangia kidogo.

Alisema maadhimisho hayo yanayofanyika baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa kuzindua rasmi Mpango wa Magonjwa Yasiyoambukiza jijini Dodoma mwaka jana.

Wiki hii ambayo ilizinduliwa Novemba 7 mwaka huu kwa matamasha ya michezo, inaadhimishwa katika mikoa yote 26 Tanzania Bara na kitaifa inafanyika katika mkoa wa Dar es Salaam katika Manispaa ya Ilala, viwanja vya Mnazimmoja.

Chanzo: habarileo.co.tz