Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watafiti wachunguza tamaduni kukithiri utapiamlo

75d815df0444a51fda4bbd94ce8abc95.jpeg Watafiti wachunguza tamaduni kukithiri utapiamlo

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (Muhas), na Chuo Kikuu cha De Montfort cha Uingereza wameanza kutafiti sababu za tamaduni za jadi zinazosababisha mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi kushindwa kutokomeza utapiamlo.

Watifiti hao ambao wanafanya kazi na serikali na washirika wengine wa maendeleo wanatarajia kwamba matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuandika upya mikakati itakayosaidia kutokomeza tatizo la utapiamlo kwenye mikoa hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya amesema leo Jumatano kuwa serikali imekuwa ikishughulikia changamoto hiyo kwa kujenga miundombinu bora kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini.

Hata hivyo, alisisitiza juhudi zaidi zinahitajika ili kutokomeza tatizo hilo la utapiamlo.

Alisema miundombinu iliyojengwa na serikali ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya, utoaji wa huduma za afya ya watoto wachanga na wajawazito.

“Kumekuwa na kampeni isiyo na mwisho ya uhamasishaji ambayo inalenga kupinga tamaduni za jadi zilizopitwa na wakati,” alisema Profesaa Mgaya.

Alisema halmashauri pia zimekuwa zikitenga bajeti mahususi kwa kuboresha lishe kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Kwa wastani ongezeko la utapiamlo lilipungua hadi asilimia 31.8 mwaka 2018 kutoka asilimia 48.3 mwaka 1999,” alisema.

Hata hivyo, Profesa Mgaya anaamini kuwa utafiti mpya utasaidia kama nchi kurekebisha sera yake katika masuala ya lishe na kuweka mikakati itakayosaidia kutokomeza tatizo hilo nchini.

Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Elimu yahya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Ama Kasangala, amekiri utafiti huo mpya utasaidia serikali na washirika wa maendeleo kufanyia kazi na kutokomeza kabisa tatizo hilo la utapiamlo.

“Inashangaza kwamba maeneo ambayo yanaripotiwa kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi ndio yana kiwango cha juu cha utapiamlo,” alisema Dk Kasangala ambaye pia ameshiriki katika utafiti huo.

Naye Profesa Gasto Frumence kutoka Muhas amesema wanalenga kuchunguza chanzo cha kuwapo kwa utapiamlo wa kiwango kikubwa katika maeneo hayo kwa kuangazia tamaduni za jadi.

“Wataalamu wa afya tunataka kuangalia tatizo lilipo na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika kutokomeza utapiamlo nchini,” alisema Profesa Frumence.

Mratibu wa Afya kutoka Mkoa wa Ruvuma, Martha Sauga alisema changamoto inayokabili mkoa huo ni uwelewa mdogo kwa watoa huduma za afya na jamii.

“Changamoto nyingine ni kwamba wadau wengi wamekuwa hawafanyi kazi katika mkoa mzima, wanachagua wilaya tatu kati ya wilaya nane za mkoa huo,” alisema.

Ruvuma ni moja ya mikoa nchini yenye viwango vya juu vya utapiamlo. Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, kati ya watoto 10, watoto wanne wana utapiamlo.

Mikoa mingine ni Iringa, Njombe na Songwe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz