Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watafiti nchini wajichimbia kutafuta chanjo ya corona

C5a09aa50c4a62e10c007f40ad490948.jpeg Watafiti nchini wajichimbia kutafuta chanjo ya corona

Sun, 8 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAFITI wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), wameanza kufanya utafiti wa chanjo ya virusi vya corona ili iweze kuzalishwa hapa nchini kwa ajili ya kukidhi mahitaji.

Makamu Mkuu wa Sua, Profesa Raphael Chibunda alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa utoaji wa chanjo ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19 kwa wafanyakazi na jamii ya chuo hicho.

Alisema lengo la kutaka kuzalisha chanjo hiyo nchini ni kutosheleza mahitaji ya nchi bila ya kutoka nje ya nchi.

Alisema chanjo zote zilizoanza kutumika nchini zimeletwa kutoka nje ya nchi, lakini wao kama wasomi hapa nchini kwa kutumia nafasi zao wakiwa sehemu ya vyuo vikuu wameona ni vyema kuanza kufanya utafiti wa pamoja na kupata chanjo ili kukidhi mahitaji ya chanjo za ugonjwa huo kwa kuzalisha hapa nchini.

“Sisi tukiwa ni sehemu ya vyuo vikuu vya nchi yetu tumeona tushirikiane na vyuo vingine vikuu kama Chuo Kikuu Muhimbili na NIMR tuanze kuzalisha chanjo yetu ya virusi vya corona ili kusaidia kupunguza makali na madhara ya virusi hivyo kwa taifa,” alisema Profesa Chibunda.

Kuhusu chanjo hiyo kwa jamii nzima ya chuo kikuu hicho, alisema baada ya chanjo hizo kuwasili mkoa wa Morogoro waliwasilisha ombi la kuwa na kituo chuoni hapo kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 15,000 na wafanyakazi 2,000 ambao wengi wao wana umri mkubwa.

Alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella na Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa huo kwa kukubali kuanzisha kituo hicho na kuwapa chanjo 500 kwa hatua za mwanzo kwa ajili ya kuchanja makundi maalumu.

Profesa Chibunda alisema pamoja na uchache wa chanjo walizopata, wana amini wataongezewa kadri siku zinavyoendelea na aliisihi jamii kupuuza na kuacha kupotoshwa na baadhi ya watu kwenye mitandao kuwa chanjo hiyo ina madhara kitu ambacho hakina ukweli.

“Maprofesa wanachanjwa hapa sasa kama hii chanjo ingekuwa na madhara yoyote wao ndio wangekuwa wa kwanza kutochanja hebu tuachane na watu wanaopotosha kuhusu chanjo hii,” alissema Profesa Chibunda.

Dktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na kiongozi wa madaktari katika hospitali ya chuo kikuu hicho, Dk Omary Kasuwi alishukuru kupatikana kwa chanjo hiyo, akisema itasaidia kupunguza changamoto za wagonjwa waliokuwa wakifika kupata matibabu katika hospitali hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz