Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu wataka bima ya afya itumike tiba asili

F76b0cc140b2da21e22bbb23de031563 Wataalamu wataka bima ya afya itumike tiba asili

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAALAMU wa tiba asili wameiomba serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iruhusu matumizi ya bima za afya kwa wananchi katika vituo vya kutolea huduma ya tiba asili.

Mtaalamu wa Tiba Asili ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo, aliyasema hayo jana alipozungumza na HabariLEO kuhusu nafasi ya tiba asili kutibu na kuponya tatizo la vidonda vya tumbo.

Mwalongo alisema tatizo la vidonda vya tumbo, linazidi kuongezeka katika jamii ya Watanzania, Afrika na duniani kwa ujumla.

Mwalongo alisema kumekuwa na kilio cha wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali nchini, kutaka watumie bima za afya wanapokwenda kupata tiba kwenye vituo vya kutolea huduma ya tiba asili ikiwemo tiba ya vidonda vya tumbo.

“Tunaiomba serikali uwekwe mfumo wa bima za afya kutumika katika vituo vya kutolea huduma vya tiba asili. Jambo hili linawezekana kama tukisimamia mwongozo wa afya, mpango kazi wa elimu, kuelimisha wataalamu na kuwarasimisha, kuzitambua dawa zote za tiba asili nchini, kuwa na viwango vya bei ya pamoja ya matibabu kwa magonjwa mbalimbali,”alisema Mwalongo.

Alisema unahitajika mkakati ikiwa ni pamoja na kubainisha mahitaji ya ajira na kuwepo kwa mfumo wa utawala katika tiba asili, kuwepo utaratibu wa kubadilishana taarifa kati ya wataalamu wa tiba asili na wataalamu katika huduma za afya za kisasa, pia uwepo ushirikiano kati ya tiba asili na tiba ya kisasa.

“Tunaweza kurekebisha mapungufu haya kwa kuweka mkakati wa pamoja wa kitaifa unaowahusisha wadau wote wa afya, wataalamu wenye uzoefu mkubwa katika tiba asili, mkakati huo utengewe bajeti ya kutosha, tuandae wataalamu na wataalamu hao wajulikane, vituo vinavyotoa huduma ya tiba asili vijulikane na viwanda vinavyozalisha dawa asili vijulikane.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba Asili ya Fadhaget Nutrition Science, Dk Fadhili Emily, alisema vidonda vya tumbo ni mchubuko wa kadiri ya nusu sentimeta katika utumbo.

Dk Fadhili alisema watu wengi wana dalili za vidonda vya tumbo, lakini wakipimwa wanaambiwa hawana kwa sababu mchubuko huo bado haujafikia ukubwa wa nusu sentimeta.

Alisema tiba asili ndiyo mwarobaini kwa tatizo la vidonda vya tumbo kwa kuwa imefanya vizuri.

“Vidonda vya tumbo visipotibiwa kwa wakati vinaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kifo. Utumbo unapopata vidonda unalika na kupata maambukizi yanayoweza kusababisha utumbu kutoboka, kusababisha upungufu wa nguvu mwilini na nguvu za kiume,” alisema Dk Fadhili na kuongeza;

“Vidonda vya tumbo visipotibiwa vinaweza pia kushusha presha au kuipandisha, kusababisha viungo vikubwa mwilini kutofanya kazi kwa ulinganifu na kusababisha ganzi miguuni, mikononi, kichwa kuuma, kupoteza uzito na kusababisha upungufu wa lishe mwilini.”

Chanzo: habarileo.co.tz