Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu waelezea undani wa watoto pacha wanaoungana

10184 PACHA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na matukio mfululizo ya kuzaliwa kwa watoto pacha walioungana, wanasayansi wamesema si jambo la ajabu, bali kuongezeka kwa mawasiliano kumechagia taarifa za matukio hayo kusambaa kwa haraka.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na la Julai 25, ambapo pacha wa jinsi ya kiume walizaliwa wakiwa wameungana moyo, ini na mshipa mkubwa wa damu mkoani Mwanza.

Jingine ni lile la Julai 12 la pacha wa jinsi ya kiume waliozaliwa wakiwa wameungana tumbo, Vigwaza mkoani Pwani huku la tatu likiwa la wale waliozaliwa Januari 29, katika Zahanati ya St Thereza Omukajunguti wilayani Misenyi.

Daktari bingwa wa watoto kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi (Muhas), Dk Francis Furia alisema kwa kawaida pacha wapo wa aina mbili.

Alisema wapo pacha wa yai moja ambalo hugawanyika mara mbili (identical twin) na wale wa mayai mawili yanayoingia kwa pamoja kwenye mfuko wa uzazi (unidentical twin).

“Sasa ikitokea lile yai halikugawanyika vizuri, yaani halikukamilika kwenye kugawanyika kwake inatokea watoto wawili wameungana sehemu fulani pale na zaidi hasa huwa tumboni,” alisema.

Dk Furia ambaye ni mhadhiri wa Muhas alisema kati ya watoto 50,000 wanaozaliwa duniani, pacha wa aina hii huzaliwa.

“Hii si ajabu na wala haitushtui, siku hizi mawasiliano yamekuwa rahisi ndiyo maana haya matukio yanafahamika.”

Alisema zamani pacha wa aina hizi walikuwa hawapati tiba nzuri na hivyo wengine waliishia kupoteza maisha na baadhi ya matukio hayakuripotiwa.

Alisema mpaka sasa hakuna sababu yoyote kimsingi inayosababisha pacha kuungana.

Hata hivyo alisema kisayansi hatua hiyo hutokea kati ya siku ya 10 hadi 13 baada ya ujauzito kutungwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Colman Living alisema tatizo hilo hutokea kijenetiki.

Alisema katika kugawanyika kuna hatua ambazo yai hutengana mapema zaidi na wakati mwingine huchelewa.

“Wanaochelewa kugawanyika ndiyo mara nyingi huungana, ni matokeo ya kuchelewa huko huungana maeneo mbalimbali ikiwamo kifua, tumbo, ubavu,” alisema.

“Tafiti zimebaini wengi wanaoungana ni wale wa jinsi ya kike.”

Hata hivyo, Dk Colman alisema hakuna dawa au mazingira yanayotajwa kuwa ndicho chanzo cha kuungana kwao.

Alisema matukio hayo yapo tangu miaka ya zamani, lakini kutokana na ongezeko la idadi ya watu na kukua kwa teknolojia imekuwa rahisi taarifa za watoto walioungana kutangazwa.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhari alisema hakuna sababu inayofahamika mpaka sasa ya kuzaliwa kwao, lakini kuna mambo yanayotajwa kusababisha hali hiyo.

Kwa mfano, alisema mjamzito kutotibu ugonjwa wa malaria na matumizi ya vyakula na vinywaji visivyo salama hasa vyenye gesi na tindikali.

“Mjamzito anatakiwa kuhudhuria kliniki mapema kwani kuna maelekezo kuhusu ale nini ambacho kitamjenga mtoto, kama vyakula vyenye calcium, protini. Atapewa dawa za folic acid ambazo zitakaza misuli ya mtoto, zinasaidia kumjenga mtoto akiwa bado tumboni,” alisema.

Pia alisema kuna dawa ambazo huzuia maambukizi ya watoto wakiwa tumboni kwani wapo wanaozaliwa wakiwa na malaria. Lakini sababu nyingine inayotajwa ni kuzaa watoto wengi kati ya sita hadi 15.

“Pia kujifungua katika umri mkubwa, lakini wakati mwingine ni matatizo ya kurithi,” alisema Dk Bokhari.

Chanzo: mwananchi.co.tz