MHADHIRI katika Idara ya Biolojia na Bioteknolojia Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Daniel Meeda amesema chanjo inayotumika nchini ya kampuni ya Johnson Johnson ni bora kuliko nyingine kutokana na mazingira yake ya uhifadhi.
Akizungumza na HabariLEO jana, Dk Maeda alisema chanjo hiyo inaweza kukaa kwenye kiwago cha baridi cha nyuzi nne ikilingalishwa na chanjo za aina nyingine. “Chanjo ya Johnson inaweza kukaa katika friji zetu za kawaida tunazoweka nyama ambayo ni nyuzi nne, lakini chanjo nyingine haziwezi kukaa kwenye kiasi hicho cha ubaridi,” alisema.
Dk Maeda alisema chanjo ya Johnson ina gharama nafuu katika usafirishaji na pia utunzaji wake ni tofauti na chanjo nyingine. “Chanjo nyingine gharama ya uhifadhi na usafirishaji ni kubwa, lakini katika kukinga zote zina ubora ndo maana zimepewa kibali na WHO ni ngumu kulinganisha moja na nyingine,” alisema na kuongeza: “Ila zote zinasaidia kwenye kulinda kupata maambukizi, nchi za watu wachache zinatumia chanjo ya aina moja lakini nyingine zinatumia chanjo zaidi ya moja.”
Alisema chanjo ya Johnson inatengezwa koti ambayo ni kirusi kisichokuwa na madhara katika mwili na ndani ya koti hiyo kunakuwa na DNA ambayo ina protini inayoongeza kinga mwilini na mfumo huo unatumika kwa chanjo nyingi na ni wa siku nyingi, hivyo kwa chanjo hiyo haina matatizo. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mapafu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Elisha Osati alisema chanjo inasaidia mtu kutokupata ugonjwa mkali ambao unaweza kumsababishia madhara makubwa.
“Chanjo za corona zinafanyakazi kuanzia asilimia 75 na kuendela, malengo mapana ya chanjo sio tu kuzuia kutokupata virusi na kukinga usipate ugonjwa mkali ili usipate madhara makubwa ambayo yanaweza kusababisha kuumwa zaidi au kufa, mapafu yakiharibika huwezi kurudi katika hali ya zamani.”
“Tahadhari ni muhimu sana ni lazima kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na kuepuka misongamano kwasababu bado maambukizi yapo na yanaweza kuenea,” alisema. Dk Osati alisema mtu anapochanja anaweza kuambukizwa tena kwani chanjo si dawa, hivyo ni muhimu watu kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya.
“Watu wanahoji kwanini mtu akipata chanjo anaweza kuambukizwa, ni hivi chanjo sio dawa, chanjo tulizonazo Tanzania ni nyingi, tunatoa chanjo 15 pamoja na ya corona,” alisema.