Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu afya wahitajika migodini

MGODI Wataalamu afya wahitajika migodini

Mon, 1 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WIZARA ya Afya imeombwa kupeleka wataalamu wa afya katika maeneo ya wachimbaji wadogo ili kutoa elimu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona, kwa kuwa kundi hilo ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini kutokana na uwepo wa mwingiliano wa watu wengi.

Ombi hilo limetolewa na wachimbaji wadogo wa eneo la Msasa wilayani Chato, mkoani Geita, wakati wakipokea vifaa vya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona vilivyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo (FADev).

Wachimbaji hao Zacharia John na Saanane Chai wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema licha ya hofu ya uwepo wa virusi vya corona kupungua nchini, lakini bado elimu ya namna ya kujikinga inahitajika kwa wachimbaji wadogo, ambao mazingira ya kazi yanamwingiliano wa watu wengi.

Katibu wa mgodi wa kilimo kwanza uliopo katika eneo hilo, Saanane Chai, alisema kauli zinazotolewa na Rais John Magufuli dhidi ya virusi vya corona imeondoa hofu iliyokuwa imetanda kwa wananchi, lakini ipo haja ya elimu ya kujikinga na maambukizo kutolewa kwenye makundi ya uchimbaji ili waweze kujikinga.

“Kama mnavyojua maisha ya wachimbaji wadogo hawana muda wa kusikiliza redio wao muda wote wako wanatafuta wakipata wanaenda kutumia kama elimu haitatolewa na bahati mbaya akapata maambukizo mchimbaji mmoja atawaambukiza wengi kutokana na mazingira ya kazi yalivyo,” alisema Chai.

Mchimbaji mwingine, Josephat Manyenye ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi katika mgodi wa Kilimo Kwanza, alisema janga la corona limesababisha biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo kuwa ngumu kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuhofia kuwekeza fedha kwenye uchimbaji.

“Ili mchimbaji mdogo aweze kufanya kazi lazima amtegemee mfanyabiashara mkubwa wa madini ambao wanatoa fedha kumuwezesha mchimbaji kuchimba akipata anamuuzia dhahabu kwa sasa wafanyabiashara wamekaa pembeni wakihofia fedha zao kutorudi hii imekua changamoto kwetu,” alisema Manyenye.

Kwa upande wake, Zagamba Mohamed, alisema janga la corona limeathiri zaidi shughuli za uchimbaji kwa kushusha uchumi na kwamba kabla ya corona mfuko wa udongo unaosadikiwa kuwa na dhahabu uliuzwa kati ya 100,000 hadi 150,000, lakini kutokana na wafanyabiashara kuhofia kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia udongo umeshuka hadi kufikia Sh. 15,000 na kuwa hasara kwa wachimbaji wadogo.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Tinna Mwasha, alisema taasisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeandaa machapisho na mabango yenye ujumbe wa namna ya kujikinga na virusi vya corona yatakayobandikwa katika maeneo ya taasisi za umma, pamoja na maeneo ya migodi ili kuisaidia jamii kupata elimu ya namna ya kujikinga na maambukizo.

Mbali na machapisho hayo pia taasisi hiyo imetoa vitakasa mikono, ndoo za maji, sabuni na barakoa kwa wachimbaji lengo ni kuwasaidia wafanye kazi katika mazingira yasiyo hatarishi na kuwataka kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ya namna ya kujikinga.

Mwasha alisema kundi la wachimbaji wadogo bado linahitaji kujengewa uwezo wa namna ya kuchimba kisasa na kufanya shughuli za uchimbaji kuwa biashara badala ya kuchimba kwa mazoea, ili kutimiza azma ya serikali kuona wachimbaji wadogo wanakuwa kiuchumi na kulipa kodi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live