Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasichana 72 wanapata Ukimwi kila siku nchini

29772 Wasicvhasna+pic Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Antony Mavunde

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Antony Mavunde amesema kwa siku wasichana 72 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU).

Akizungumza juzi katika kilele cha shughuli za vijana kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma jana, Mavunde alisema wasichana hao ni kati ya vijana 90 wenye umri huo ambao wanapata maambukizi mapya kwa siku moja.

Alisema takwimu hizo zilizotokana na utafiti wa viashiria vya Ukimwi wa mwaka 2016/17, zinaonyesha vijana 90 ni kati ya watu 225 wanaopata maambukizi mapya kila siku nchini.

“Takwimu hizi zinaashiria jambo moja kubwa kuwa endapo hatutachukua hatua kukabiliana na hali hii mapema, maambukizi ya VVU yatazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka na hivyo kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa ifikapo 2030 kusiwe na maambukizi mapya kabisa,” alisema.

Takwimu hizo zimewashtua wadhibiti wa ugonjwa huo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema takwimu hizo ni changamoto kwa malengo yao ya 2030.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alisema vijana hawawezi kutatua matatizo kwa kujidanganya kuwa hayapo na badala yake watambue kuwa Ukimwi upo na wajielekeze kupata elimu sahihi jinsi ya kujikinga na kuishi maisha marefu kama watakuwa wameambukizwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz