Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapendekeza kupima sikoseli kabla ya ndoa iwe lazima

Ndoa Siko Cell Mapendekezo hayo yameungwa mkono na baadhi ya wajumbe

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kupambana na ugonjwa sikoseli unaowatesa wakazi wa mikoa ya Kanda Ziwa, wadau wa afya mkoani Mwanza imependekeza kupitishwa kwa sheria kwa wachumba wanaotarajia kufunga ndoa kupima ugonjwa huo ili kupunguza idadi ya watu wanaougua maradhi hayo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachuzibwa amesema tatizo la ugonjwa wa sikoseli kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ni kubwa.

Dk Rutachuzibwa ameyazungumza hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza , ameshauri kuwepo kwa sheria ya lazima itakayotumika kupata cheti cha taarifa ya vipimo vya ugonjwa huo kama ilivyo kwa ugonjwa wa Ukimwi kabla ya wachumba kuruhusiwa kufunga ndoa.

“Katika siku za hivi karibuni, tumefanya tafiti kwenye kitengo chetu cha damu salama na kubaini vimelea vya ugonjwa wa sikoseli ni vikubwa, hivyo ni vyema sheria ya kupima ugonjwa huo kwa wanandoa iwe ya lazima ili kupunguza tatizo hilo,” amesema Dk Rutachuzibwa.

Kauli hiyo imeungwa mkono na wajumbe wa wa kamati hiyo ambao wamesema sheria hiyo ianze kutekelezwa mara moja ili kupunguza tatizo hilo.

“Hili jambo si la kuchelewa lipitishwe na lianze kutekelezwa mara moja ili kupunguza kizazi kinachoweza kutokana na sikoseli, kwasababu wanandoa wasipopimwa wanaweza kuwa na chembechembe zinazochangia kuzaa watoto wenye ugonjwa huo,” amesema Antipas Mgungusi, Mbunge jimbo la Malinyi.

Katika hatua nyingine kamati hiyo imeshauri uongozi wa mkoa na watendaji wengine kuongeza nguvu katika kukabiliana na maambukizi mapya ya Ukimwi ili kufikia azma ya Serikali ya kupunguza maambukizi hayo na kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Fatuma Taufiq amesema hali ya maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Mwanza inatisha na inafikia kwenye takwimu za kitaifa za asilimia 7.2 na kwamba mikakati zaidi iongezwe katika kukabiliana na changamoto hiyo.

“Mwanza mna kazi kubwa ya kuhakikisha mnapunguza maambukizi ya ugonjwa huo, mje na mikakati utakaosaidia kushusha takwimu hizo, viongozi na watendaji washughulikie suala hilo ambalo linawakumba zaidi wanawake,” amesema Taufiq.

Hata, hivyo mganga mkuu wa mkoa amebainisha mikakati inayotumika ni pamoja na kugawa mipira ya kiume (kondomu) kwenye maeneo ya mialo, mahoteli, na kumbi za starehe ili kukabiliana na tatizo hilo lakini pia kutoa dawa kwa wavuvi.

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Pindi Chana amewataka viongozi kuhakikisha wanaisaidia jamii kupunguza maambukizi ya ya Ukimwi.

“Jambo la kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni jambo nyeti, na hili lipewe kipaumbele hususani tunapoelekea kwenye sensa ya watu na makazi, watu wahesabiwe lakini pia waelimishwe kuhusu maambukizi hayo ili kufikia azma ya Serikali ya kupunguza magonjwa hayo,” amesema Pindi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live