Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake, watoto walioathiriwa na majanga ya moto kufanyiwa upasuaji bure

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na shirika la madaktari bingwa wa upasuaji wanawake itafanya upasuaji kwa wanawake 46 walioathirika na ajali za moto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, mkuu wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Athar Ali alisema shughuli hiyo ambayo ni bure itahusisha wanawake na watoto waliopata ajali na majanga ya moto.

Amesema wanawake ni wahanga wakubwa katika jamii kwa ukatili na majanga mengine ndio maana shughuli hiyo imelenga wanawake na watoto wa kike.

“Ushirikiano wetu unalenga kuwahudumia wanawake na watoto wa kike waliopata majanga ya moto, ajali pamoja na ukatili,” alisema Dk Athar.

Dk Edwini Mrema daktari bingwa kutoka MNH alisema ushirikiano huo ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita umeanza kuonyesha mafanikio kutokana na idadi ya wanaohitaji huduma hiyo kuongezeka kila mwaka.

Alisema mwanzoni watu walikuwa hawajui wakipata majanga ya moto wapi waende lakini kutokana na ushirikiano umeweza kuwanufaisha wengi.

Kwa upande wake, daktari bigwa wa upasuaji kutoka Marekani, Dk Andrea Pusic alisema ameridhishwa na kazi inayoendelea hasa ya kuelimisha waathirika hao pamoja na kuwajengea uwezo madaktari.

“Niwashukuru madaktari kwa namna wanavyowatafuta waathirika hao pamoja na elimu wanayoitoa, ni vigumu kuwatafuta wagonjwa wa namna hii,” alisema.

Dk Pusic alisema wanawake wengi wanapata majeraha makubwa wakati wa majukumu yao ya kuhudumia familia upasuaji huo umelenga wanawake na watoto wa kike.

Katika zoezi hilo linalofadhiliwa na wadau mbalimbali gharama za upasuaji kwa kwa jumla wanawake 46 ni Sh268 milioni, ambapo madaktari bingwa 20 watashirikiana kutoa huduma hiyo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz