Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wanaolea watoto bila wenzi wao waongezeka kwa kasi

26526 Pic+watoto TanzaniaWeb

Sun, 11 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hali ya mtoto kulelewa na mzazi mmoja hasa wa kike ilikuwa kawaida katika karne ya 17 na 18.

Sababu kubwa ilikuwa ni vifo, ambavyo sehemu kubwa vilitokana na maradhi, vita na ajali za barabarani.

Pia matibabu duni yalichangia vifo vingi wakati huo.

Mbali na vifo vilivyosababishwa na malazi, wakati huo ajali za barabarani pia ziliacha familia nyingi zikibaki na mzazi mmoja. Mataifa mengi pia yalikuwa yakipigana vita wakati huo na hii inatajwa kuwa sababu nyingine iliyoacha familia nyingi zikibakiwa na mlezi mmoja.

Inakadiriwa kuwa wakati huo, mtoto mmoja kati ya watatu walilelewa na mzazi mmoja baada ya mwenzi wake kufariki.

Hata hivyo, kuimarika kwa miundombinu, kusitishwa kwa vita na kuimarika kwa huduma za afya kumechangia kupungua kwa vifo hasa katika umri wa ujana katika karne ya 20 na 21.

Vifo vya mzazi mmoja vinavyotokana na kukosekana kwa huduma stahiki za matibabu, vimepungua na badala yake talaka, watoto wanaotokana na mimba zisizotarajiwa au kutaka kuwa mzazi kwa hiyari kumechangia ongezeko la idadi ya wazazi wanaolea watoto bila ya wenzi wao.

Utafiti uliofanywa na shirika linaloshughulikia ustawi wa watu duniani, OECD, mwaka jana, unaonyesha kuwa asilimia 17 ya watoto walio katika umri wa kuanzia miaka 0 hadi 14, wanaishi na mzazi mmoja.

Utafiti huo unaonyesha kuwa waathirika wakubwa ni wanawake ambao ni asilimia 88 ya wazazi wanaolea watoto bila ya wenzi wao wa kiume.

Idadi ya familia zinazoishi na mzazi mmoja inaongezeka, hasa katika maeneo ya mijini na aina hii ya familia inakubalika katika maeneo mengi ya mijini tofauti na vijijini.

Nchi za China, Iran, India, Indonesia, Israel, Jordan na Uturuki-- kwa mujibu wa machapisho mbalimbali ya Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), OECD, DHS na Benki ya Dunia (WB)-- zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoelelwa na mzazi mmoja.

Taarifa hizo zinaonyesha kuwa kwa wastani zaidi ya asimilia 10 ya watoto katika mataifa hayo, wanalelewa na mzazi mmoja, idadi ambayo ni theluthi moja ya familia za aina hii duniani kutoka katika nchi hizo.

Nchini Afrika Kusini, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 40 ya watoto wanaishi na mama pekee, wakati ni asilimia nne tu wanaoishi na baba pekee.

Nchi zinazofuata kwa familia za mzazi mmoja barani Afrika ni Msumbiji ambayo ni asilimia 36, Dominican (35), Liberia (31) na Kenya (30).

‘Yapo mambo mazuri pia’

Mtaalamu wa saikolojia na ushauri, Dk Chris Mauki anasema takwimu za sasa ulimwenguni zinaonyesha ongezeko kubwa la watoto wanaolelewa na kukuzwa na mzazi mmoja tofauti na mila na tamaduni za miaka ya nyuma kwamba malezi ya mzazi mmoja yanaonekana kukubalika.

Pamoja na kuwa ni mtindo unaoshamiri, Dk Mauki anasema hakuna mtoto anayetamani kukuzwa au kulelewa na mzazi mmoja, bali hulazimishwa na mazingira.

Anasema yapo baadhi ya mambo yanayosababisha hali ya mtoto kuwa na mzazi mmoja na mara nyingine haiepukiki.

“Yapo mambo mazuri pia ambayo mtu anaweza kujifunza kutokana na kuwa mzazi peke yake,” anasema Dk mauki.

“Kwa mfano; mara nyingine mzazi anayelea na kukuza mtoto au watoto peke yake anaweza kugundua uwezo (mtoto) alionao ndani yake ambao asingeweza kuufahamu kama wangekuwa wazazi wawili.

“Wengi wamejikuta wana uwezo wa kujituma zaidi na kufanya zaidi pasipo kuwa tegemezi, tofauti na wanapokuwa na mzazi mwingine.

“Wengine wamejifunza kuwa furaha ya kweli haitokani au kuletwa na mtu mwingine, bali inachochewa na mtu mwenyewe kutokea ndani yake. Nafahamu ukweli kwamba kulea mtoto au watoto peke yako si kazi rahisi lakini pia upo ukweli kwamba ziko baadhi ya faida kama utakubaliana na changamoto.”

Wanawake wenye kipato wameamua

Ni dhahiri kuwa kuna athari za mzazi mmoja kulea mtoto peke yake, hasa kama mama au baba atafanya hivyo kwa kulazimishwa na mazingira na si hiari yake.

Mtaalamu wa sosholojia wa mkoani Morogoro, Mbago Urio anasema utamaduni wa familia kulelewa na mzazi mmoja unashika kasi, lakini wapo wanaolazimishwa na mazingira na hawa ndio wanaoathirika.

Anasema wanawake wengi wenye kipato kikubwa wameamua kulea watoto peke yao na kwamba hiyo haina madhara kwa kuwa familia inapata mahitaji yote muhimu, kama elimu nzuri.

“Wanawake watu wazima wenye vipato vikubwa wapo wengi katika kundi hili la wanaolea watoto peke yao, ukiwatazama hawa, utagundua kuwa familia hazikosi kitu, mama anakuwa na muda wa kuwaangalia watoto na kuwapatia mahitaji muhimu kwa sababu pia amepevuka kiakili,” anasema.Kuhusu wanaotelekezwa, anasema: “Tatizo ni pale mama anapokimbiwa na mpenzi au mume na kubaki na watoto peke yake. Huyu akiwa hana uwezo anaweza kuwa chanzo cha familia isiyo na ustawi mzuri.”

Anaongeza kuwa mama au baba wa aina hii pia huwa anahitaji ushauri wa kisaikolojia kwa sababu wengi hupatwa na msongo wa mawazo, kuwa na hasira na mwisho wa siku huhamishia hasira kwa watoto.

Hawafanyi vizuri darasani

Kuhusu masomo, anasema mara nyingi watoto wanaolelewa na mama au baba kutokana na kulazimishwa na mazingira, huwa hawafanyi vizuri darasani.

“Mama au baba anakuwa na jukumu la kutafuta mahitaji muhimu ya watoto, kutokana na kuelemewa anatumia muda mwingi kujitafutia mkate wa kila siku. Hapati muda wa kutosha kukaa na watoto kufuatilia masomo yao,” anasema.



Chanzo: mwananchi.co.tz