Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake walivyoshika usukani kuongoza wizara za afya Afrika Mashariki

50928 Pic+wanawake

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji wa masuala ya afya bila shaka utabaini kuwepo kwa mabadiliko mengi katika sekta hiyo nchini na hata kwa nchi jirani miaka ya hivi karibuni.

Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakiongelewa na kufanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa ni uboreshwaji wa huduma za afya hasa upande wa afya ya mama na mtoto.

Lakini umeshawahi kufahamu nini kilicho nyuma ya hilo? Kwa taarifa yako walioshika usukani kuongoza sekta ya afya katika nchi za Afrika Mashariki ni wanawake.

Wizara za afya katika nchi nne ikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda zinaongozwa na wanawake isipokuwa Sudan Kusini na Burundi ambako hata hivyo awali iliongozwa na mwanamke.

Kinachosisimua zaidi mawaziri hao ni wanasheria kitaaluma huku wawili wakiwa ni madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto na upasuaji.

Mwananchi linakuletea orodha yao na dondoo kadhaa kuwahusu na nyadhifa mbalimbali walizowahi kushika kabla ya kuongoza wizara hiyo.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Tanzania)

Ni mbunge wa Viti Maalum kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ameshika nyadhifa ya kuwa Waziri wa Afya tangu mwaka 2015 alipoteuliwa na Rais John Pombe Magufuli na amekaa vipindi viwili bungeni.

Ummy ambaye ni mwanasheria pia ana shahada ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria aliyoipata mwaka 2001. Kati ya mwaka 2000 na 2010 amekuwa akifanya kazi katika mashirika mbalimbali ya serikali na yasiyo ya serikali yanayohusika na masuala ya sheria, utafiti na utawala.

Katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete amewahi kusimamia wizara kadhaa katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2014 alikuwa Naibu Waziri katika wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Pia amewahi kuwa Naibu waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Sheria na Katiba.

Mwaka 2015, Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Afya nafasi anayoitumikia mpaka sasa na kuwa miongoni mwa mawaziri wachache waliodumu katika wizara tangu uteuzi wa awali.

Akiwa waziri wa afya amehimiza kuzuia mimba na ndoa za utotoni kwa kupelekwa muswada bungeni na baadaye kuwa sheria. Mbali na hayo ameonyesha juhudi katika mambo mengi ikiwemo kuhakikisha anaweka nguvu katika kutokomeza vifo vya mama na mtoto.

Sicily Kanini Kariuki – Waziri wa Afya Kenya

Ni mwanasiasa kutoka nchini Kenya ambaye anaongoza Wizara ya Afya tangu mwaka 2018. Kabla ya kupewa nafasi hiyo kuiongoza alikuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia tangu mwaka 2015 mpaka Januari 2018 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Afya.

Kariuki aliyezaliwa katika kijiji cha Al-Kalou, Kaunti ya Nyandarua, ana shahada ya kwanza kutoka chuo kikuu cha Nairobi. Shahada ta Uzamili ya usimamizi wa biashara aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha ESAMI kwa kushirikiana na shule ya usimamizi wa biashara Maastricht iliyopo Netherlands.

Pia, ana stashahada ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani.

Kariuki amefanya kazi nyingi zihusuzo biashara ikiwamo kuwa Ofisa wa Mamlaka ya Uwekezaji nchini Kenya na Afisa Mkuu wa Fresh Produce Exporters Kenya.

Pia, amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji na CEO wa Bodi ya Chai Kenya. Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Idara ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini humo.

Desemba 2015, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia alipotumikia hai kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Afya 2018.

Dk Jane Aceng – Waziri wa Afya Uganda

Kitaaluma ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto lakini pia mwanasiasa nchini Uganda. Ni Waziri wa Afya katika bunge la Uganda. Aliteuliwa kushika wadhifa huo Juni 6 mwaka 2016.

Kabla ya hapo, Juni mwaka 2011 mpaka Juni 2016 alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu katika Wizara ya Afya nchini humo.

Dk Aceng ana shahada ya udaktari na shahada ya upasuaji lakini pia ana shahada ya uzamili ya udaktari wa watoto na shahada ya uzamili ya udaktari zote alizipata kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Makerere.

Lakini pia ana stashahada ya uongozi na utawala kutoka chuo cha Uganda Management Institute.

Nyota yake iling’aa tangu akiwa Wizara ya afya alipoteuliwa Mkurugenzi Mkuu wa huduma za madawa lakini pia ameshawahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Lira.

Dk Diana Gashumba – Waziri wa Afya Rwanda

Kitaaluma ni daktari bingwa wa watoto kutoka nchini Rwanda, mwanasiasa na kiongozi wa Afya. Ni Waziri wa Afya kutoka bunge la Rwanda ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo Oktoba 4 mwaka 2016.

Kabla ya hapo, Machi 26 mwaka 2016 mpaka Oktoba 4 mwaka 2016, alikuwa waziri wa Jinsia na (Gender and Family promotion)

Diana ambaye ni mcheshi wakati wote, ana shahada ya udaktari na shahada ya uzamili katika udaktari lakini pia ni daktari bingwa wa watoto.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, Dk Gashumba amefanya kazi ya udaktari kwa miaka 17 kabla ya mwaka 2016.

Kwa kipindi cha miaka mitatu alikuwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kibagabaga na Hospitali ya Muhima. Kati ya mwaka 2010 na 2016, alifanya kazi na USAID katika programu ya afya ya mama na mtoto akiwa kiongozi wa kitengo hicho.



Chanzo: mwananchi.co.tz