Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake 600 wanaoishi na VVU kupimwa saratani 

Ad92ba9febbfd8b69ceb9eaac296a825 Wanawake 600 wanaoishi na VVU kupimwa saratani 

Tue, 5 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ZAIDI ya wanawake 600 mkoani Kagera watanufaika na mradi wa kuhamasisha wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi (VVU) wapime saratani ya mlango wa kizazi hadi Desemba, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Jumanne Isango, alisema hayo wakati akizindua mpango huo, mjini hapa juzi.

Alisema saratani ya mlango wa kizazi ni hatari kwa wanawake wanaoishi na VVU.

Isango alisema Tacaids kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uwezeshaji Wanawake (UN-Women), inatekeleza mradi wa uhamasishaji wanawake hasa wanaoishi na VVU wachunguze saratani ya mlango wa kizazi mkoani Kagera.

Alisema wameanza katika kata tano za Bukoba Vijijini na wanatarajia ikifika Desemba mwaka huu wanawake 600 watakuwa wamechunguzwa saratani ya mlango wa kizazi.

Isango alisema wanawake 25 kutoka Shirika la Wanawake Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi mkoani Kagera (Amwavu), wamepatiwa elimu kuhusu dalili za saratani.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Meja Jenerali Charles Mbuge, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali, alisema watahakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwani walikuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika lisolo la kiserikali la Amwavu ambao ndio watekelezaji wa mradi huo, Gasper Lutainulwa, alisema upo uhusiano kati ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na VVU.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Safina Yuma, alisema ingawa mwanamke yupo hatarini kupata saratani ya mlango wa kizazi, lakini wenye VVU wapo kwenye hatari zaidi hivyo waende kupima kwani kuna vituo takribani 700 nchini vinavyotoa huduma hiyo bila malipo.

Mratibu wa Programu za Ukimwi na Jinsia kutoka UN-Women, Jacob Kayombo, alisema wameona watoe mchango kudhibiti saratani ya mlango wa kizazi ili kusaidia juhudi za serikali kuimarisha afya za wananchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz