Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume watakiwa kujichunguza saratani ya matiti

82132 Saratani+pic Wanaume watakiwa kujichunguza saratani ya matiti

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanaume nchini wametakiwa kuwa na utamaduni wa kujichunguza matiti kubaini viashiria vya saratani kwani kuchelewa kugundua ugonjwa huo kunapunguza uwezekano wa tiba.

Wito huo umetolewa na daktari bingwa wa saratani, Sikudhani Muya wakati wa uchunguzi wa saratani ya matiti na utoaji elimu ya ugonjwa huo uliofanyika jana katika hospitali ya Mloganzila kuadhimisha mwezi wa utoaji wa elimu ya ugonjwa huo.

Wakati Dk Muya akieleza hayo, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema Serikali imeelekeza nguvu katika kupambana na saratani ya matiti kwa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa huku akiwataka wanaume wanaojihisi viashiria vya ugonjwa huo kufika kwenye vituo vya afya.

“Saratani ya matiti kwa wanaume ni aghalabu, inaweza kutokea ukapata mgonjwa mmoja kwa miaka 10, lakini wanawake ni tatizo linalowasumbua zaidi,” alisema.

Dk Muya alieleza kuwa licha ya wanawake kuwa waathirika wakubwa wa saratani ya matiti wapo pia wanaume wanaopata ugonjwa huo, lakini huchelewa kujigundua kutokana na maumbile yao.

Alisema hilo linawafanya kufika hospitali wakiwa katika hatua mbaya kutokana na kuchelewa kupata matibabu.

“Wengi wanajua saratani ya matiti ni kwa wanawake pekee, ukweli ni kwamba hata wanaume wanaweza kuwa na tatizo hili. Inaweza kuwa ngumu kwao kugundua haraka kwa sababu matiti yao hayana nyama hivyo kushindwa kuona dalili kwa haraka ila wakipimwa wanaweza kubaini tatizo,” alisema Dk Muya.

Kuhusu aina hii ya saratani kwa wanawake, alisema imeendelea kuwa tishio huku idadi kubwa wakizidi kugundulika kuwa na tatizo hilo linalogharimu maisha.

Alipoulizwa juu ya ugonjwa huo, Denis Ruhindwa, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam alisema, “Sifahamu kama saratani ya matiti inaweza kumpata mwanaume, ninachojua ni tatizo la wanawake.”

Naye Khamis Magitu mkazi wa Kijitonyama alieleza kuwa na ufahamu kuhusu ugonjwa huo kwa wanaume na amewahi kufanya uchunguzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz